
SIKU chache baada ya kumalizika kwa msimu wa 2013/2014, hatimaye
Kocha Mkuu wa Yanga, Hans van Der Pluijm amekamilisha ripoti yake na
kuiwasilisha kwa uongozi wa timu hiyo.
Pluijm ambaye alichukua jukumu la kuinoa timu hiyo wakati wa katikati
ya msimu uliopita, ameonyesha kuwa mkali na ambaye anahitaji kufanya
vizuri zaidi msimu ujao baada ya kushika nafasi ya pili katika msimu
huu.
Ripoti hiyo ya kocha huyo ambayo Championi Jumamosi
imepata dondoo zake ni kuwa amepanga kuwa na sura mpya kadhaa na pia
wale ambao wataonekana hawana faida kwake na hawamo kwenye mipango yake,
ameruhusu waondoke na hayo yatatendeka ikiwa uongozi wa klabu yake
utayafanyia kazi.
Baadhi ya wachezaji waliomo kwenye kikosi hicho ambao ameruhusu
waondoke kwa sababu mbalimbali ni Haruna Niyonzima, Athumani Idd
‘Chuji’, Jerry Tegete, Shaban Kondo, Rajab Zahir, Ibrahim Job, Salum
Telela na Ally Mustapha ‘Barthez’.
Mtoa taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo amelithibitishia gazeti hili kuwa, hao ni baadhi yao ambao wametajwa kwenye ripoti hiyo.
“Niyonzima anaondolewa kwa kuwa kocha hamhitaji kwenye mipango yake,
Chuji sababu kubwa ni utovu wa nidhamu, hao wengine ni suala la
viwango,” alisema mtoa taarifa.
Kitu cha ajabu kilichoibuka kwenye ripoti hiyo ni kuwa kocha huyo
amesema anamhitaji mshambuliaji Reliants Lusajo ambaye mara nyingi
amekuwa ‘bize’ na shule kiasi cha kushindwa kuonekana mara kwa mara
kwenye timu.
“Amesema anamtaka Lusajo, sababu kubwa ni kuwa ana kiwango kizuri
licha ya kuwa hajacheza mechi nyingi lakini pia ana elimu nzuri, anajua
anaweza kuwa kioo kwa wachezaji wengine,” alisema mtoa taarifa huyo.
Pluijm, raia wa Uholanzi, ambaye juzi alikuwa Uwanja wa Taifa,
akifuatilia mchezo wa kujipima nguvu baina ya timu ya taifa ya vijana
(U-20) dhidi ya Taifa Stars, alizungumza na gazeti hili na kuweka wazi
mambo kadhaa.

Kipa wa Yanga, Ally Mustapha ‘Barthez’.
“Kuhusu ripoti yangu, hilo ni suala langu na utawala wa klabu, labda
cha kukwambia ni kwamba watu watarajie kuona sura mpya nyingi msimu ujao
na kuna sura hazitakuwemo, lakini hayo yatafanyika iwapo ripoti
niliyowasilisha itafanyiwa kazi vilivyo,” alisema Mholanzi huyo.
Aidha katika ripoti hiyo haijamzungumzia mshambuliaji Mganda Emmanuel
Okwi, ambaye aliweka mgomo wa kutocheza mechi za mwisho za ligi kuu kwa
madai kuwa hajamaliziwa fedha zake za usajili, japokuwa kiongozi huyo
alishatanza kuwa Okwi, hayumo kwenye mipango yake msimu ujao.
Post a Comment