Logarusic aiacha Simba afuata timu Kenya, Ghana

HAMUELEWEKI tatizo. Kocha wa Simba, Zdravko Logarusic haelewi lolote kuhusu mkataba wake mpya utakaomuwezesha kuendelea kuifundisha klabu hiyo, ameamua kuondoka zake kwenda Kenya kisha Ghana alikoitwa na rafiki zake.
Wiki chache zilizopita Logarusic raia wa Croatia, alizungumza na Mwanaspoti akilalamikia kitendo cha Simba kumpiga danadana kuhusu mkataba mpya hadi wiki iliyopita kupewa sharti la kuifunga Yanga katika mchezo wa juzi Jumamosi ili apewe mkataba mwingine.
Mkataba wa sasa wa kocha huyo unaisha mwezi ujao, lakini ni kama umeisha kwani Simba haina michuano yoyote itakayoshiriki ndani ya siku zilizobaki hadi kocha huyo atakapomaliza siku zake za kuitumikia timu hiyo.
Jana Jumapili, Logarusic alisema hajui lolote juu ya hatma yake ndani ya timu hiyo na akaenda mbali kwa kusema amebakiza siku tano za kubaki nchini na kujua kama ataendelea kuinoa timu yake au vinginevyo.
Logarusic ambaye katika mechi ya juzi almanusura mbinu zake ziwalaze mapema mashabiki wa Yanga katika mchezo wa Ligi Kuu Bara baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1, alisema hakuna kiongozi yeyote wa Simba aliyemfuata kuzungumza naye kuhusu mkataba  mpya.
Alisema ndani ya siku chache zijazo ataondoka kuelekea Kenya na Ghana kuwatembelea rafiki zake, lakini zikitimia siku tano yaani Ijumaa ya wiki hii atakuwa amejua Simba haina mpango naye na atajiunga na timu nyingine itakayomuhitaji ndani na nje ya Tanzania.
“Nitakuwepo Tanzania hadi Jumatano au Alhamisi mapema, baada ya hapo nitaenda Kenya halafu Ghana ambako rafiki zangu wameniita, ikifika siku ya tano ambayo ni Ijumaa bila ya Simba kuniambia lolote nitajua mimi na wao hatuna kitu cha kuendelea kutufanya tuwe pamoja.
“Silazimishi Simba wanipe mkataba lakini sitaki kuonekana nina tamaa ya fedha kwa kwenda timu nyingine bila ya wao kuniambia kitu, mimi sasa ni kama kocha huru ninayeweza kujiunga na timu yoyote.
“Kuhusu kitakachotokea nikiwa Kenya au Ghana siwezi kukuthibitishia lakini mimi kama kocha ajira yangu ni soka, nikipata timu siwezi kukataa maana ndiyo maisha yangu,” alisema Logarusic.
Ukweli wa mambo
Mwanaspoti lina uhakika kuwa, Logarusic anaenda Kenya kufanya mazungumzo na klabu za Gor Mahia na AFC Leopards ambazo zilionyesha nia ya kumsajili ili aweze kuifundisha mojawapo ya timu hizo zinazoshiriki Ligi Kuu Kenya.
Kama mambo hayataenda vizuri na moja kati ya klabu hizo za Kenya, Logarusic ataenda Ghana kufanya mazungumzo na klabu ya Accra Hearts of Oak inayotafuta kocha kwa nguvu zote.
 mwanaspoti

Post a Comment

Previous Post Next Post