Mtoto
wa marehemu anayejulikana kwa jina la Abdalah aliliambia Uwazi kuwa
siku mauti yalipomfika baba yake katika wodi namba sita Jengo
la Mwaisela, alimtembelea na kumkuta akiwa katika hali nzuri na
alipopewa chakula alikula, akashiba lakini cha ajabu alisema hatakula
tena.
Kijana huyo alisema muda mfupi baadaye, hali ya baba yake
ilibadilika, akaanza kupumua kwa shida ndipo alipozidiwa na baadaye
kukata roho.
Mwanamuziki nguli wa muziki wa dansi nchini, Muhidini Maalim Gurumo
aliyefahamika pia kama kamanda na mashabiki wa muziki wa dansi, aliyeaga
dunia Jumapili iliyopita katika Hospitali ya Muhimbili jijini Dar,
alikutana na mateso ya kwa saa 72 za mwisho wake baada ya kulazwa akiwa
taabani kwa siku tatu.
Mzee Gurumo alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa mapafu kwa muda mrefu na aliwahi kulazwa katika hospitali hiyo ya Muhimbili.
Baadhi ya watu waliomtembelea mzee Gurumo kwa nyakati tofauti akiwa
hospitalini hapo ni pamoja na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania,
Dk. Jakaya Mrisho Kikwete ambaye alimuombea afya njema na akaruhusiwa
kurudi nyumbani.
Kifo chake kimeacha simanzi si tu kwa familia yake, bali kwa wadau wa
muziki wa dansi kwani alikuwa mwalimu na kiongozi wa wanamuziki wengi
ambao sasa wanatamba.
Baada ya kustaafu muziki, Mzee aliwahi kupewa
zawadi ya gari na msanii wa Bongo Fleva, Naseeb Abdul ‘Diamond Platnumz’
aina ya Toyota Funcargo.
Akizungumzia msiba huo, Kiongozi wa Bendi ya Extra Bongo, Ally Choki
alisema wamempoteza mwalimu wa muziki asiyekuwa na choyo ya kuelimisha.
“Ni kama tumepoteza tochi tukiwa kwenye msitu mnene usiku wa manane,” alisema.
Naye msemaji wa Bendi ya Mlimani Park Ochestra (Sikinde Ngoma ya Ukae),
Jimmy Chika alipozungumza na Uwazi alisema mzee Gurumo aliwahi
kuja kuwatembelea na kuimba mwezi mmoja uliopita katika Ukumbi wa DDC,
Kariakoo jijini Dar.
“Alikuja kama mara tatu hivi ukumbini, naona alikuwa kama anatuaga
kwa sababu alikuwa mwanzilishi wa bendi na mbunifu wa mtindo wa Sikinde,
aliubuni Septemba, 1978,” alisema Chika.Mzee Kassim Mapili, mwanamuziki
wa mkongwe, kwa upande wake alisema kifo cha Gurumo ni pengo kubwa
ambalo haliwezi kuzibika na akafafanua kuwa ni mtu ambaye hakuwa
mbinafsi.
Baadhi ya wanamuziki ambao amefanya nao kazi kwa karibu ambao sasa
watakuwa wanamlilia mwalimu wao ni pamoja na Hassan Rehani Bitchuka,
Said Mabela, Roman Mng’ande ‘Romario’ na wengine wengi.
Gurumo pia ameacha simanzi katika miji mbalimbali nchini kwa kuwa
amewahi kutembelea kimuziki na alifanikiwa kujizolea mashabiki lukuki.
Hadi Uwazi linakwenda mitamboni msiba ulikuwa nyumbani kwake
Mabibo, Dar huku taratibu za mazishi zikifanyika. Ameacha mjane na
watoto wanne.
Mungu ailaze roho ya marehemu maali pema peponi. Amina.
Credit: Gazeti la Uwazi/ GPL

إرسال تعليق