Mambo ya Muungano ya Uratibu - Zitto

Rasimu ya Katiba iliyotolewa na Tume ya Katiba imeainisha masuala saba ya Muungano. Hata hivyo masuala haya hayatoi nguvu ya kikatiba kwa Jamhuri ya Muungano kubakia moja na imara.

Masuala ya Muungano ndiyo yanayoweza kuamua hatma ya Muungano. Ni muhimu kuhakikisha Dola inakuwa imara na ya kutegemewa na Washirika.

Masuala kadhaa hayana budi kuongezwa kwenye mambo ya Muungano. Haya yaitwe masuala ya uratibu (concurrent matters) ambayo yatafanywa kwa pamoja na Serikali ya Muungano na Serikali za Washirika.

1) Usimamizi wa Hifadhi ya Jamii (social security) ni suala linahusu uhai wa Taifa na wananchi wake. Pia Hifadhi ya

Jamii ni kama Deni la Taifa (obligation of the State), kwa hiyo ni vema liwe suala la Muungano. Kila nchi Mshirika anaweza kuwa na Shirika lake la Hifadhi ya Jamii, lakini usimamizi wa Sekta ni vema ufanywe na chombo cha Muungano. Vile vile Usimamizi wa masuala ya Bima na Mabenki yanapaswa kuwa masuala ya Muungano. Masuala ya Sera za Fedha ‘Monetary policy’ huko tunakokwenda, mambo ya Umoja wa Sarafu (monetary Union) ni ya Afrika Mashariki, hivyo suala hili halina budi kuwa suala la Muungano.

2) Usimamizi na udhibiti wa Sekta ya Nishati (Mafuta na Gesi Asilia na masuala ya Atomiki) yanapaswa kuwa masuala ya Muungano. Kila nchi Mshirika anaweza kuwa na kampuni yake ya Taifa ya Mafuta na Gesi lakini masuala ya usimamizi wa sekta ni vema yawe chini ya chombo cha Muungano ili kuhakikisha kuwa utajiri wa nchi unanyonywa kwa uendelevu na pia kutoa mamlaka kwa Bunge la Muungano kupitisha/kuidhinisha mikataba ya kuvuna rasilimali hizo za Mafuta na Gesi. Ni vema pia kuwa na sera moja ya masuala ya atomiki na nyuklia kwa Jamhuri ya Muungano. Itakuwa ni mchanganyiko mkubwa kwa kila nchi Washirika kuwa na sera yake ya nyuklia.

3) Usimamizi na Udhibit wa Anga ni jambo la kuangalia upya. Rasimu ya Katiba imeondoa suala la usimamizi na udhibiti wa anga kwenye masuala ya Muungano. Nadhani ni vema kuhakikisha kuwa ‘avition, civil and military’ yanakuwa ni masuala chini ya mamlaka ya Jamhuri ya Muungano. Kila nchi inaweza kuwa na Shirika lake la ndege ‘usafiri wa anga’ lakini masuala ya usimamizi na udhibiti wa anga yabakie kuwa masuala ya Muungano. Muungano utakuwa na mashaka makubwa sana siku Mshirika akiruhusu anga yake kutumika na maadui au nchi zenye misimamo tofauti na Tanzania. Ili kuzuia mkanganyiko wowote unaoweza kutokea ni vema masuala ya udhibiti wa anga yakawa masuala ya Muungano.

4) Usimamizi na Udhibiti wa Mawasiliano ya Simu ni jambo la Muungano. Hivi sasa Tanzania nzima inatumia nambari +255 kuitambulisha katika masuala ya mawasiliano ya simu. Rasimu ya Katiba imeondoa suala la mawasiliano ya simu katika orodha ya masuala ya Muungano. Nadhani ni makosa makubwa sana. Suala la usimamizi na udhibiti wa mawasiliano linapaswa kubakia kuwa suala la Muungano na Tanzania nzima ibakie na +255 chini ya mamlaka ya Jamhuri ya Muungano. Rasimu itatupelekea kuwa na ‘code’ nambari nyingine kwa Tanganyika, nyingine kwa Zanzibar!

5) Masuala ya Biashara ya Kimataifa na Forodha ni masuala yanayoratibiwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki hivi sasa na hivyo haikuwa sawa kuyaondoa kwenye masuala ya Muungano. Kwa mfano, hivi sasa Bunge la Tanzania au la Uganda au la Burundi hayana mamlaka kabisa kwenye masuala ya forodha maana Bunge la Afrika Mashariki ndio lenye mamlaka hayo na hutunga Sheria ya forodha (Customs Management Act, 2004). Afrika Mashariki ipo kwenye Umoja wa Forodha na kuelekea Soko la Pamoja, hivyo kuondoa forodha na biashara ya kimataifa kwenye masuala ya Muungano ni kutoona mbali.

Zitto Kabwe

Post a Comment

Previous Post Next Post