AFRIKA Mashariki ukitafuta ni kocha yupi anasifika kwa mipango
uwanjani kama ilivyo kwa Jose Mourinho wa Chelsea ya Uingereza utatajiwa
jina la Sredojevic Milutin ‘Micho’ wa Uganda na Zdravko Logarusic wa
Simba.
Logarusic sasa ameanza mipango yake ya msimu ujao
anakotaka kurudisha heshima ya klabu hiyo, ametaka kuajiriwa kwa
mtaalamu mmoja anayeitwa Mikael Igendia spesho kwa wachezaji wake.
Unajua kwa nini? Logarusic raia wa Croatia
ameitumikia Simba kwa miezi sita na baadaye akagundua jambo moja kubwa
kwamba shida moja iliyokisumbua kikosi chake ni kutokana na kuona
wachezaji wake wakikosa mazoezi mazuri ya kisasa ya viungo.
Kulimaliza tatizo hilo tayari ameshaliweka katika
ripoti yake aliyoikabidhi kwa Katibu Mkuu wa Simba, Ezekiel Kamwaga,
kocha huyo ametaka klabu hiyo kufanya maboresho katika benchi lake la
ufundi kuajiriwa kwa Igendia ambaye ni maalumu kwa kazi hiyo.
Igendia ambaye ni raia wa Kenya aliwahi kufanya
kazi na Logarusic wakiwa Gor Mahia ya Kenya ambapo kutokana na kuyajua
majukumu yake hayo, kocha huyo ametaka Simba imuwahi haraka mtaalamu
huyo aweze kutua Simba msimu ujao ambao amesema utakuwa na mapambano ya
kweli.
Akizungumza na Mwanaspoti, Logarusic alisema Simba
ikimaliza kumleta Igendia itakuwa imepunguza majukumu kwa makocha wa
kikosi hicho ambapo mtalaamu huyo atakuwa na kazi ya kuwaweka sawa
wachezaji wao kimwili kabla ya kuanza kupokea mbinu mbalimbali.
Logarusic alisema kwa sasa Igendia anamalizia
mafunzo maalumu nchini Norway ambapo ameitaka Simba kuhakikisha inaanza
mawasiliano naye haraka muda wowote akigusa ardhi ya Kenya.
“Nataka huyo mtu aje (Igendia) namjua vizuri hasa
uwezo wa kazi yake, tumekuwa tukipata shida hasa katika kuwandaa
wachezaji, nataka kuona kila kitu kinafanyika kitaalamu msimu ujao,
tukimpata Igendia tutakuwa tumefanya jambo zuri,” alisema Logarusic.
Akimzungumzia Igendia, Katibu Mkuu wa Gor Mahia,
George Bwana alisema anamjua vizuri Igendia ambaye ana asili ya Finland
ambapo amesema mtalaamu huyo ni kati ya watu wazuri wanaoweza kuwandaa
wachezaji ambaye kwa sasa amemaliza mafunzo yake na anatafuta kazi ya
kufanya.
“Hatukuwa na mkataba na Igendia alivyokuwa hapa
Gor (Mahia), kama Logarusic akimpata nafikiri atakuwa amefanya kitu
kizuri kwa timu yake ni kijana mdogo anayejua kuwatengeneza wachezaji,
alipokuwa hapa alitufanyia kazi nzuri sana, nimezungumza naye hivi
karibuni ameniambia amemaliza mafunzo na sasa anatafuta kazi ya kufanya,
waambie Simba wamuwahi haraka,” alisema Bwana.
Chanzo:- Mwanaspoti
Chanzo:- Mwanaspoti
إرسال تعليق