![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEhr_kPehPULKxFwySKyPlkqZl5YT_l2BEB9NnKpU0pCTIrLw2kAx4cyTrnAU-cUSciM28uzj8AUp0pAVQtQCXjIJMcBleIcxMP1H5kaH4j2SyaVnzAkx2_gvGX-P011ulj87bv0jcfeHmI/s1600/1.jpg)
Baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani wametoa sababu zilizowafanya wasihudhurie sherehe za maadhimisho ya miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Katika sherehe hizo zilizofanyika Jumamosi katika
Uwanja wa Uhuru, viongozi wa vyama vikuu vya upinzani, Chadema, CUF na
NCCR-Mageuzi hawakuonekana.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alisema
kutokuonekana kwao hakuna uhusiano na msimamo wa chama wala Ukawa kama
inavyodhaniwa.
“Mwenyekiti wangu (Freeman Mbowe), alikuwa
safarini na kazi zake zote nazifanya mimi. Hata kama angekwenda uwanjani
mimi nisingekwenda kabisa,” alisema.
Alisema alishaamua kutokwenda katika sherehe
zozote za kitaifa kama maadhimisho ya Uhuru wa Tanganyika na Muungano
tangu mwaka 2012 kutokana na sherehe hizo kugharimu fedha nyingi ambazo
zingetumika katika maendeleo.
Alitaja sababu nyingine kuwa ni kuhusishwa na masuala ya kisiasa hususan chama tawala cha CCM.
Naibu Mkurugenzi wa Haki za Binadamu, Habari na
Uenezi (CUF), Abdul Kambaya alisema chama chake kiliamua viongozi wote
kutokuhudhuria sherehe hizo kutokana na kukosekana kwa maridhiano ya
kujadili Rasimu ya Katiba inayozungumzia muundo wa Muungano.
Alisema chama kiliona hakuna sababu ya viongozi
wake kuhudhuria sherehe za Muungano ambao majadiliano juu ya muundo wake
yameshindwa na wajumbe wa Bunge Maalumu wameng’ang’ania muundo wa
serikali mbili ambao haumo kwenye Rasimu.
“Wananchi wangetushangaa tumetoka bungeni juzi tu hapa halafu tunahudhuria sherehe za Muungano wenye makovu,” alisema Kambaya.
Alisema hakuna kiongozi wa chama chake
aliyehudhuria katika sherehe hizo zaidi ya Katibu Mkuu wake, Seif Sharif
Hamad ambaye alikwenda kwa shughuli za kiserikali akiwa Makamu wa
Kwanza wa Rais wa Zanzibar.
Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Mosena Nyambabe
alisema viongozi wa chama chake hawakuhudhuria kutokana na sababu zao
binafsi... “Hatukukaa kama chama wala Ukawa kujadili kwamba tusihudhurie
sherehe hizo,” alisema
Post a Comment