Mkazi
wa Kijiji cha Lubungo wilayani Mvomero, Juma Mbega, amekutwa amekufa na mwili
wake kuharibika nyuma ya Kituo Kikuu cha Polisi mkoani Morogoro.
Akizungumza
na mwandishi jana baada ya kugundulika kwa mwili wa Mbega, mjukuu wa marehemu
Nuru Adam, alisema kwa muda mrefu babu yake huyo alitoweka nyumbani kwao.
Kwa
mujibu wa Adam, babu yake huyo alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kuanguka,
ambao ulisababisha augue ugonjwa wa akili na muda mwingi alikuwa akiingia
kwenye maofisi na migahawani kuomba fedha na chakula.
Alisema
mara ya mwisho alionekana akifanyakazi ya kumenya viazi katika mabanda ya
chipsi kwa ujira wa fedha kidogo na chipsi, na nyakati za usiku alikuwa akilala
kwenye baraza za maduka maeneo ya mjini.
Nuru
alisema yeye na ndugu zake walishindwa kumhudumia babu yao kwa kuwa yeye
mwenyewe alikuwa akigoma kurudi nyumbani.
Baadhi
ya mashuhuda waliokuwepo jirani na eneo hilo, walidai walimuona babu huyo wiki
iliyopita na jana walianza kusikia harufu ikitokea kwenye kichaka nyuma ya
Kituo kikubwa cha Polisi.
Kwa
mujibu wa mashuhuda hao, baadaye walipata taarifa kupitia
mtu
aliyekuwa akiokota chupa za plastiki, kwamba ameona mwili wa binadamu
ukiwa umeharibika na habari zilipofika Polisi, askari walifika na kuchukua
mwili wa babu huyo.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonard Paulo, alisema uchunguzi wa
kifo hicho unaendelea na mwili wa Mbega umeshakabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya
maziko.
Post a Comment