Akizindua kampeni hiyo Makao Makuu ya Benki hiyo jijini Dar es Salaam
jana, Ofisa Mtendaji Mkuu, Mark Wiessing alisema mbali ya upatikanaji
wa huduma haraka, kampeni hiyo itawezesha huduma kupatikana muda wowote
na mahali popote.
“Leo tunayo furaha kuzindua Kampeni hii ya Jihudumie ambapo NMB
inaendelea kubuni na kuongeza huduma ambazo mteja anaweza kuzipata bila
kwenda katika tawi la NMB.
“Tunapenda kuwafahamisha wateja wetu kwamba sasa wanaweza kupata huduma
za benki yetu kwa njia zao wenyewe zilizounganishwa na mtandao wa simu
ya mkononi na njia nyingine mbadala kama mashine za ATM, huduma za benki
kwa njia ya intaneti, PesaFasta na Akaunti ya Chap Chap,” alisema
Wiessing.
Alisema kupitia kampeni hiyo, NMB imeweza kuzingatia mahitaji ya msingi
ya wateja wake, ikiwemo uhakika wa huduma za kibenki na uwezo wa
kuzipata wakati wowote na mahala popote.
“Kwa kubonyeza tu kitufe cha simu, fedha itaweza kutoka kwenye akaunti
yako ya NMB kwenda mahala pengine popote kama vile kwenye malipo ya
LUKU, kulipia muda wa maongezi wa simu na hata kuweza kutoa kiasi
kinachofikia Sh milioni moja kupitia mashine za ATM,” alisema.
Baadaye wakizungumza katika Benki ya NMB Tawi la Kariakoo, wakati wa
mwendelezo wa uzinduzi huo uliofanywa kwa matawi yote ya benki hiyo
jijini Dar es Salaam, wateja wa benki hiyo walisifia kampeni hiyo,
wakisema imelenga kuwapunguzia adha, usumbufu na kuokoa muda wa kupata
huduma za kibenki.
“Ni huduma nzuri na tunawashukuru NMB kwa kuanzisha kampeni hii. Kwa
mfano leo nitajiunga na huduma za Jihudumie na kuanzia kesho nitaweza
kufanya shughuli zote za kibenki nikiwa nyumbani au mahala pengine
popote bila kulazimika kufika hapa,” alisema Mathias Haule.
Mary Chilewa alisema huduma hiyo itawanufaisha wateja na pia itaiwezesha
benki hiyo kuwa bora zaidi, kwa vile fedha zilizokuwa zinatumika
kujenga matawi ili kuhudumia wateja, zitatumika sasa kutoa mikopo ya
masharti nafuu kwa wananchi wa kipato cha chini.
“Ni huduma nzuri sana maana wateja hatutakuwa na ulazima tena wa kufika
kwenye matawi, tutafanya huduma za kibenki sisi wenyewe na hivyo yale
mabilioni ya fedha waliyokuwa wanayatumia kujengea matawi ili
kutuhudumia sasa watakuwa hawana pa kuyapeleka bali kutukopesha sisi
wajasiriamali kama mikopo nafuu,” alisema Chilewa.
Post a Comment