BENKI YA NMB YAZINDUA HUDUMA YA JIHUDUMIE

Benki ya NMB imezindua kampeni mpya ya Jihudumie, yenye lengo la kuwezesha upatikanaji wa haraka wa huduma mbalimbali za benki hiyo.

Akizindua kampeni hiyo Makao Makuu ya Benki hiyo jijini Dar es Salaam jana, Ofisa Mtendaji Mkuu, Mark Wiessing alisema  mbali ya upatikanaji wa huduma haraka, kampeni hiyo itawezesha huduma kupatikana muda wowote na mahali popote.

“Leo tunayo furaha kuzindua Kampeni hii ya Jihudumie ambapo NMB inaendelea kubuni na kuongeza huduma ambazo mteja anaweza kuzipata bila kwenda katika tawi la NMB.

“Tunapenda kuwafahamisha wateja wetu kwamba sasa wanaweza kupata huduma za benki yetu kwa njia zao wenyewe zilizounganishwa na mtandao wa simu ya mkononi na njia nyingine mbadala kama mashine za ATM, huduma za benki kwa njia ya intaneti, PesaFasta na Akaunti ya Chap Chap,” alisema Wiessing.

Alisema kupitia kampeni hiyo, NMB  imeweza kuzingatia mahitaji ya msingi ya wateja wake, ikiwemo uhakika wa huduma za kibenki na uwezo wa kuzipata wakati wowote na mahala popote.

“Kwa kubonyeza tu kitufe cha simu, fedha itaweza kutoka kwenye akaunti yako ya NMB kwenda  mahala pengine popote kama vile kwenye malipo ya LUKU, kulipia muda wa maongezi wa simu na hata kuweza kutoa kiasi kinachofikia Sh milioni moja kupitia mashine za ATM,” alisema.

Baadaye wakizungumza katika Benki ya NMB Tawi la Kariakoo, wakati wa mwendelezo wa uzinduzi huo uliofanywa kwa matawi yote ya benki hiyo jijini Dar es Salaam,  wateja wa benki hiyo walisifia kampeni hiyo, wakisema imelenga kuwapunguzia adha, usumbufu na kuokoa muda wa kupata huduma za kibenki.

“Ni huduma nzuri na tunawashukuru NMB kwa kuanzisha kampeni hii. Kwa mfano leo nitajiunga na huduma za Jihudumie na kuanzia kesho nitaweza kufanya shughuli zote za kibenki nikiwa nyumbani au mahala pengine popote bila kulazimika kufika hapa,” alisema Mathias Haule.

Mary Chilewa alisema huduma hiyo itawanufaisha wateja na pia itaiwezesha benki hiyo kuwa bora zaidi, kwa vile fedha zilizokuwa zinatumika kujenga matawi ili kuhudumia wateja, zitatumika sasa kutoa mikopo ya masharti nafuu kwa wananchi wa kipato cha chini.

“Ni huduma nzuri sana maana wateja hatutakuwa na ulazima tena wa kufika kwenye matawi, tutafanya huduma za kibenki sisi wenyewe na hivyo yale mabilioni ya fedha waliyokuwa wanayatumia kujengea matawi ili kutuhudumia sasa watakuwa hawana pa kuyapeleka bali kutukopesha sisi wajasiriamali kama mikopo nafuu,” alisema Chilewa.

Post a Comment

أحدث أقدم