Dodoma. Tuhuma za ufisadi wa zaidi ya Sh200
bilioni katika akaunti ya Escrow ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT)
zinaonekana kuwa kaa la moto na jana zilitikisa Bunge na kuibua mvutano
mkali.
Hata hivyo, suala hilo sasa limekabidhiwa kwa
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ili kubaini ukweli wake.
Tuhuma hizo ziliibuliwa juzi na Mbunge wa Kigoma
Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi), ambaye alisema kashfa hiyo ni
zaidi ya ile ya Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ya BoT iliyotokea mwaka
2005.
Kafulila alisema ufisadi huo unamhusisha Waziri wa
Nishati na Madini, Waziri wa Fedha, Mwanasheria Mkuu wa Serikali,
Gavana wa BoT na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme (Tanesco).
Ingawa Kafulila hakutaja kwa majina, Waziri wa
Nishati ni Profesa Sospeter Muhongo, wa Fedha ni Saada Mkuya, Katibu
Mkuu wa wizara hiyo (Nishati) ni Eliakim Maswi na AG ni Frederick
Werema.
Hata hivyo, akihitimisha hotuba ya bajeti yake na
kujibu hoja mbalimbali za wabunge, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alimwagiza
CAG na Takukuru kuchunguza tuhuma hizo ili kubaini ukweli.
“Hoja iliyopo na inayoleta ubishani ni kuondoa
pesa kutoka akaunti ya Escrow na kuzipeleka IPTL. Tunajiuliza kama ni
ufisadi, ni ufisadi wa nini wakati fedha zile ni za IPTL?” alihoji
Pinda.
Pinda alifafanua suala hilo lilipoandikwa kwa
kirefu na gazeti dada la Mwananchi (The Citizen), CAG aliwasiliana na
Katibu Mkuu wa Nishati, Gavana wa BoT na Mkurugenzi wa Tanesco ili
kupata picha ya mchakato mzima.
“Wakati akiendelea hivyo, CAG akapata barua kutoka
kwa Katibu Mkuu wa Nishati akimwomba afanye uchunguzi wa kina na wakati
huo huo kamati ya PAC nayo ikamwelekeza kuchunguza jambo hilo.”
Waziri Mkuu aliongeza kusema: “Kwa tuhuma zenyewe
zilivyo, itabidi tuwahusishe Takukuru nao wafanye kazi kwa upande wao
ili kupata ukweli.
“Kwa maelezo na mtiririko ulivyo, kinachobaki ni
tuhuma zinazojitokeza ambazo upo uwezo mkubwa wa vyombo hivi kuweza
kuzibaini. Naliomba Bunge lako likubali CAG akubali kukamilisha kazi
hiyo.”
Waziri Mkuu alisema wako viongozi wa Serikali
ambao wametuhumiwa katika suala hilo hivyo ni vyema likachunguzwa kwa
uzito wake ili wale watakaobainika wamekula rushwa washtakiwe.
- Mwananchi
- Mwananchi
إرسال تعليق