Rais Jakaya Kikwete,
amewaahidi wafanyakazi nchini kuwa mambo mazuri yakiwemo ya kupanda kwa
mishahara na kupunguzwa kwa kodi ya mishahara maarufu kama Paye.
Alisema hayo akihutubia kwenye Maadhimisho ya Siku ya
Wafanyakazi Duniani Dar es Salaam leo.
“Najua hiki ndio kilio chenu na wote mnasubiria kwa hamu
Serikali inasema nini? Nawaahidi kuwa katika hotuba ya Bajeti Waziri wa Kazi na
Ajira, itabainisha wazi, kiwango cha mshahara ambacho Serikali imekiongeza
katika mishahara ya wafanyakazi,” alisema Rais Kikwete.
Hata hivyo, alisema Serikali haitoweza kupandisha mishahara
hiyo na kufikia ombi la Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA), la Sh 750,000.
Pamoja na hayo, Rais Kikwete alionyesha kutoridhishwa na namna
sehemu kubwa ya sekta binafsi, isivyozingatia viwango vya mishahara vinavyopangwa
na Serikali, hali inayochangia kuibuka kwa migogoro ya mara kwa mara baina ya
waajiri na waajiriwa.
Akizungumzia suala la Kodi ya Mapato (P.A.Y.E), Rais Kikwete,
alisema ombi hilo nalo kama ilivyo nyongeza ya mishahara ni la muda mrefu, na kuwaahidi
wafanyakazi hao kuwa nalo linafanyiwa kazi ili kupunguza kutoka asilimia 13
inayotozwa kwa sasa na kufikia tarakimu moja.
Naye Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudentia Kabaka, alimpongeza
Rais Kikwete kwa kupatiwa tuzo ya utawala bora Afrika, na kuwataka waajiri
nchini kutumia fursa hiyo kumuenzi kiongozi hiyo kwa kuhakikisha wanafuata
nyayo na kusimamia utawala bora, ili kupunguza migogoro ya kazi.
Katibu Mkuu wa Tucta, Nicholaus Mgaya, akiwasilisha risala ya
wafanyakazi katika maadhimisho hayo, aliiomba Serikali ishughulikie matatizo
yanayowakabili wafanyakazi ya uboreshaji wa mishahara, kupunguzwa kwa kodi ya
P.A.Y.E na kuboreshewe pensheni.
Post a Comment