Kiingilio
cha chini cha mechi ya kwanza ya raundi ya mchujo kuwania tiketi ya
kucheza Fainali za Afrika 2015 nchini Morocco kati ya Tanzania (Taifa
Stars) na Zimbabwe (Mighty Warriors) itakayochezwa Jumapili (Mei 18
mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ni sh. 5,000.
Washabiki watakaolipa kiingilio
hicho ni kwa wale watakaokaa kwenye viti vya rangi ya chungwa, bluu na
kijani. Kwa upande wa VIP B na C kiingilio kitakuwa sh. 10,000 wakati
kwa VIP A itakuwa ni sh. 20,000.
Tiketi zinatarajiwa kuanza kuuzwa
siku moja kabla ya mechi hiyo katika vituo mbalimbali jijini Dar es
Salaam, na uwanja siku ya mchezo huo utakaoanza saa 10 kamili jioni.
Taifa Stars inayodhaminiwa na
Kilimanjaro Premium Lager ikiwa chini ya Kocha Mart Nooij inatarajia
kurejea jijini Dar es Slaam kesho (Mei 14 mwaka huu) kutoka Mbeya
kuendelea na maandalizi ya kuikabili Zimbabwe.
RAMBIRAMBI MSIBA WA MKUFUNZI KASINDE
Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko kifo cha Mkufunzi wa waamuzi
nchini, Omari Kasinde kilichotokea jana (Mei 12 mwaka huu) jijini Dar es
Salaam.
Mbali ya kuwa Mkufunzi, Kasinde
ambaye anazikwa leo (Mei 13 mwaka huu) mchana katika Makaburi ya Kisutu,
Dar es Salaam pia alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati iliyopita ya
Waamuzi ya TFF iliyokuwa chini ya uenyekiti wa Kapteni mstaafu Stanley
Lugenge.
Msiba huo ni mkubwa katika fani ya
mpira wa miguu nchini kwani, Kasinde enzi za uhai wake alitoa mchango
mkubwa katika mchezo huu tangu akiwa mwamuzi na baadaye mkufunzi na
kiongozi..
TFF tunatoa pole kwa familia ya
marehemu Kasinde, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA),
na Chama cha Waamuzi wa Mpira wa Miguu Tanzania (FRAT) na kuwataka kuwa
na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.
Bwana alitoa, Bwana ametwaa jina lake lihimidiwe. Amina.
BONIFACE WAMBURA
OFISA HABARI NA MAWASILIANO
SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)
إرسال تعليق