Mkutano
wa 15 wa Bunge la Bajeti, unaingia wiki ya pili ya vikao vyake, ambavyo wizara
zinawasilisha bajeti zake huku leo Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na
Mazingira zikiwasilisha bajeti zake.
Bunge
hilo lililoanza Mei 6 na kutarajiwa kuahirishwa Juni 27, linaendelea na vikao
wakati wizara saba zikiwa zimeshawasilisha na kupitisha bajeti zake.
Wizara
ambazo tayari bajeti zake zimeshapitishwa ni Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera,
Uratibu na Bunge; Uwekezaji na Uwezeshaji na Tawala za Mikoa na Serikali
za Mitaa.
Nyingine
ni Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma; Utawala Bora na Mahusiano na
Uratibu. Pia Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika bajeti yake ilipitishwa
juzi.
Kwa
upande wa wizara zinazowasilisha leo bajeti zake zilizo chini ya Ofisi ya
Makamu wa Rais, ya Muungano inatarajiwa kutawaliwa na mjadala mkubwa
utakaojielekeza kwenye yaliyojiri Bunge Maalumu la Katiba.
Hii
inatokana na hali halisi iliyojitokeza katika bunge maalumu la katiba, ambako
suala la Muungano liliibua mjadala mkubwa uliosababisha baadhi ya wajumbe chini
ya umoja wao wa Ukawa kususia.
Katika
mjadala wa leo, upo uwezekano mkubwa wa masuala ya Bunge Maalumu la Katiba
kujadiliwa zaidi, ikizingatiwa kwamba Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani,
Freeman Mbowe alifungulia njia kupitia hotuba yake wakati wa kujadili
bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
Kitendo
cha Mbowe kutumia sehemu kubwa ya hotuba yake kuzungumzia masuala ya
Bunge la
Katiba, kilisababisha majibizano kutoka kwa baadhi ya wabunge wa chama tawala
wakati wa kujadili bajeti hiyo.
Ukawa
ambao kupitia kwa Mbowe juzi wamesisitiza kutorejea kwenye Bunge Maalumu la
Katiba, wabunge wake ambao ni kutoka Chadema, CUF na NCC-Mageuzi, wanatarajiwa
kutumia bunge hili kuwasilisha dukuduku zao juu ya yaliyojiri kwenye bunge
maalumu.
Hata
hivyo, baada ya hotuba hiyo ya kiongozi wa upinzani kutumia bunge hilo
kuzungumzia masuala ya katiba, waliibuka baadhi ya wabunge wa chama tawala
waliowahoji ni kwa nini walisusa bunge maalumu ambalo ndilo muafaka kujadili
masuala hayo.
Katika
hatua nyingine, kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na ofisi ya Bunge, leo saa
1:00 usiku pia Wizara ya Maji inawasilisha bajeti yake ambayo itajadiliwa
na kupitishwa kesho.
Post a Comment