LEO MKUTANO WA BUNGE LA BAJETI KUENDELEA

Mkutano wa 15 wa Bunge la Bajeti, unaingia wiki ya pili ya vikao vyake, ambavyo wizara zinawasilisha bajeti zake huku leo Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira zikiwasilisha bajeti zake.
Bunge hilo lililoanza Mei 6 na kutarajiwa kuahirishwa Juni 27, linaendelea na vikao wakati wizara saba zikiwa zimeshawasilisha na kupitisha bajeti zake.
Wizara ambazo tayari bajeti zake zimeshapitishwa ni Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge; Uwekezaji na Uwezeshaji na Tawala za Mikoa na Serikali za  Mitaa.
Nyingine ni Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma; Utawala Bora na Mahusiano na Uratibu. Pia Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika bajeti yake ilipitishwa juzi.
Kwa upande wa wizara zinazowasilisha leo bajeti zake zilizo chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais, ya Muungano inatarajiwa kutawaliwa na mjadala mkubwa utakaojielekeza kwenye yaliyojiri Bunge Maalumu la Katiba.
Hii inatokana na hali halisi iliyojitokeza katika bunge maalumu la katiba, ambako suala la Muungano liliibua mjadala mkubwa uliosababisha baadhi ya wajumbe chini ya umoja wao wa Ukawa kususia.
Katika mjadala wa leo, upo uwezekano mkubwa wa masuala ya Bunge Maalumu la Katiba kujadiliwa zaidi, ikizingatiwa kwamba Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani, Freeman  Mbowe alifungulia njia kupitia hotuba yake wakati wa kujadili bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
Kitendo cha Mbowe kutumia sehemu kubwa ya hotuba yake kuzungumzia masuala ya
Bunge la Katiba, kilisababisha majibizano kutoka kwa baadhi ya wabunge wa chama tawala wakati wa kujadili bajeti hiyo.
Ukawa ambao kupitia kwa Mbowe juzi wamesisitiza kutorejea kwenye Bunge Maalumu la Katiba, wabunge wake ambao ni kutoka Chadema, CUF na NCC-Mageuzi, wanatarajiwa kutumia bunge hili kuwasilisha dukuduku zao juu ya yaliyojiri kwenye bunge maalumu.
Hata hivyo, baada ya hotuba hiyo ya kiongozi wa upinzani kutumia bunge hilo kuzungumzia masuala ya katiba, waliibuka baadhi ya wabunge wa chama tawala waliowahoji ni kwa nini walisusa bunge maalumu ambalo ndilo muafaka kujadili masuala hayo.
Katika hatua nyingine, kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na ofisi ya Bunge, leo saa 1:00 usiku  pia Wizara ya Maji inawasilisha bajeti yake ambayo itajadiliwa na  kupitishwa kesho.

Post a Comment

أحدث أقدم