Tanzania
imesaini mikataba minne na Jumuiya za Kimataifa na wadau wa kuhifadhi
mazingira, kwa ajili ya kupambana na ujangili na uhalifu wa wanyamapori katika
hifadhi na mbuga za wanyama nchini Tanzania.
Mikataba
hiyo iliwekwa saini juzi jioni kati ya Serikali ya Tanzania na Shirika la
Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Taasisi ya Kimataifa inayosimamia Hifadhi
(ICCF-Group), Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB), Umoja wa Ulaya (EU), Benki ya
Dunia na nchi za China, Ufaransa, Ujerumani na Norway.
Mikataba
hiyo ni matokeo ya Mkutano wa Kimataifa wa Kuzuia Uhalifu wa Wanyamapori
na kuendeleza Uhifadhi wa Mazingira, uliofanyika kwa siku mbili jijini Dar es
Salaam na kushirikisha viongozi wa Serikali, jumuiya za kimataifa,
wafanyabiashara na wadau wengine katika sekta ya utalii na maliasili
Walioshiriki
katika utiaji saini ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu na
Kiongozi wa UNDP, Hellen Clerk ambapo mkataba huo ni kwa ajili ya Mfuko wa
Pamoja wa Kuhifadhi Mazingira.
Mkataba
wa pili na wa tatu, ulisainiwa kati ya Wizara ya Maliasili na Utalii,
ICCF-Group na UNDP. Mikataba hiyo ni ya makubaliano kuwa Tanzania, ifanye
mkutano wa Kanda Oktoba mwaka huu na
mwakani ifanye Mkutano wa Mapitio
ya
Utekelezaji ya Makubaliano yaliyotokana na mkutano huo.
Mkataba
wa nne ulikuwa kwa ajili ya ushirikiano baina ya Tanzania na washirika wa
kimataifa, kupambana na kuzuia uhalifu wa wanyapori na waliotia saini ni Waziri
Mkuu Mizengo Pinda, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu na kwa upande
wa washirika wa kimataifa walikuwa ni mwakilishi wa UNDP, ADB, Benki ya Dunia
na mabalozi wa China, EU, Ufaransa, Ujerumani na Norway.
Akitoa
hotuba ya kufunga mkutano huo wa siku mbili, Pinda alisema kampeni ya
kupambana na ujangili Tanzania na nchi zilizoathiriwa, haiwezi kufanikiwa
ikifanya peke yake, kwani hilo ni tatizo la dunia linalohitaji dunia nzima
kushirikiana.
Pinda
alisema zinahitajika juhudi za pamoja, kukabiliana na tatizo hilo katika
maeneo wanakoishi na wasikoishi tembo
nchini na katika bara la Afrika.
Alishukuru
wadau wa kimataifa kwa kushiriki mkutano huo na kuomba washirika wa ndani na wa
kimataifa, kufanya kazi na Tanzania kukabiliana na tatizo hilo la ujangili na
biashara haramu ya wanyamapori na kusisitiza suala la kuharibu mitandao ya
majangili.
Pinda
alisema mkutano huo, unadhihirisha
urafiki na ushuhuda wa namna wadau wote walivyojizatiti kwa ajili ya
uhifadhi endelevu na kwamba kampeni ya kupambana na ujangili, inahitaji kuwa
endelevu mpaka mwisho ushindi upatikane.
Waziri
Mkuu aliahidi washirika na marafiki wa Tanzania katika mapambano dhidi ya
ujangili, kuwa Serikali itatumia msaada wowote, uliotolewa kwa ajili ya
kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa katika mkutano huo, kwa ajili ya kuzuia
ujangili na biashara haramu ya wanyamapori.
"Kwa
kuwa kazi bado ni kubwa mbele, nachukua nafasi hii kuomba wadau wote wa ndani
na wa nje, kuendelea kusaidia juhudi za Tanzania kukabiliana na ujangili na
biashara haramu ya wanyamapori," alisema.
Mkuu
wa UNDP, Hellen Clerk alizitaka serikali duniani kote kuongeza mapambano dhidi
ya ujangili wa tembo na biashara haramu ya bidhaa za wanyamapori kama meno ya
tembo.
Clerk
alisema uhalifu unaotokana na biashara ya pembe za ndovu, una madhara makubwa
kwa watu wanaoishi katika mazingira magumu katika nchi zinazoendelea kwa
kuliibia Taifa utajiri wake, kuharibu maliasili kwa ajili ya kizazi kijacho,
kuchochea uhalifu, rushwa na kudhoofisha usalama wa jamii na taifa.
"Vitendo
hivi vya uhalifu vinawaweka wanawake, watoto na wengina katika hali ya
umasikini na maisha magumu na yaliyo na hatari," alisema.
Clerk
alisema sheria zenye nguvu na zinazotekelezeka zinahitajika, ili kupunguza
mahitaji ya bidhaa haramu za wanyamapori na jamii kufanya shughuli za
kujiimarisha na kujipatia kipato Tanzania na nchi zingine zenye tembo na
wanyamapori.
Alisema
shirika lake limejizatiti kusaidia juhudi za kupambana na biashara ya
wanyamapori kwa kusaidia utawala bora, utekelezaji wa Sheria, kupunguza
umasikini na kulinda mazingira kwa kushirikiana na serikali na washirika wengine.
"Uimarishaji
wa utawala bora ni muhimu katika kukabiliana na biashara haramu ya pembe za
ndovu na utekelezaji wa sheria unapaswa kufanywa katika eneo husika na
kuimarisha mfumo wa kitaifa," alisema.
Nyalandu
alisema ni kazi kubwa, kukabiliana na magenge ya majangili na hivyo kuna
mahitaji mkubwa wa msaada kutoka kwa jumuiya ya kimataifa na washirika wengine.
"Haya
makundi yapo hapa, kwa sababu kuna mahitaji ya bidhaa hizo kutoka nchi
nyingine. Kwa hiyo ni suala la dunia nzima kushirikiana na kuhakikisha makundi
haya yanatokomezwa kabisa na biashara hii inaondolewa kabisa," alisema na
kuongeza kuwa Serikali iko madhubuti kuhakikisha inafanya kila iwezalo kuzuia
ujangili.
Post a Comment