Mbunge
wa Ubungo, John Mnyika ameshauri bajeti ya Wizara ya Maji isisomwe leo
bungeni, badala yake irudishwe kwenye kamati ya bajeti waifumue kwa
kuiongezea fedha.
Katika
mkutano na waandishi wa habari jana mjini hapa, Mnyika alisema
bajeti ya mwaka unaomalizika haikutekelezwa kwani asilimia 27 ya
fedha zilizopangwa, ndizo zimetolewa.
Mnyika
ambaye ni Kaimu Kiongozi wa Upinzani Bungeni, alisema amebaini hayo kupitia
randama za wizara hiyo zilizowasilishwa juzi bungeni.
Alisema
leo anamwandikia Waziri wa wizara hiyo, Profesa Jumanne Maghembe
kumshauri asisome bajeti hiyo na wakati huo huo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
inakaa kikao kujadili namna ya kuzuia bajeti hiyo isisomwe.
Alisema
mradi wa Programu ya Vijiji 10 kila halmashauri pamoja na Mpango Maalumu wa
Maji wa Jiji la Dar es Salaam haijatekelezwa, licha ya serikali katika bajeti
iliyopita kuahidi kuitekeleza katika bajeti hii.
“Tulipewa
matumaini katika Bunge la Bejeti lililopita kwamba bajeti ya Wizara
ya Maji imeongezwa. ..tulipewa matumaini hewa kwamba bajeti
imeongezwa mpaka bilioni 312.1 sawa na nyongeza ya asilimia 123 ikilinganishwa
na bajeti ambayo ilitangulia ya Sh bilioni 140.1,” alisema Mnyika.
Hata
hivyo Mnyika alisema randama iliyotolewa bungeni juzi, inasema kulingana na
changamoto ya upatikanaji wa fedha, upande wa fedha za ndani kiasi
kilichotolewa ni Sh bilioni 86 pekee sawa na asilimia 27.6 ambazo kati ya hizo,
Sh bilioni 44.8 zimepelekwa kwa maji vijijini.
Alisema
mradi wa maji wa vijiji 10 kila halmashauri umetengewa Sh bilioni 34 pekee.
Alisema kiwango cha fedha kilichotolewa kwa mradi huo hakifiki hata theluthi
moja ya kiasi kilichotengwa ikizingatiwa mwaka wa fedha unaisha Juni 31.
Alisema
sehemu kubwa ya miradi vijijini haijakamilika hadi leo. “Tunajadili vipi bajeti
mpya wakati ambapo bajeti iliyotangulia utekelezaji ni finyu,” alihoji.
Natoa
mwito kwa wananchi, na wabunge wengine kuunga mkono kuhakikisha bajeti ya
wizara ya maji haijadiliwi kesho. Alisema kama Waziri Maghembe atapuuza
kutosoma bajeti, atalazimika kumtaka ajiuzulu na Waziri Mkuu ndiye afanye kazi
ya kuondoa hoja kuipeleka kwenye kamati ya bajeti.
Alipoulizwa
ni nini yeye pamoja na upinzani watafanya iwapo bajeti hiyo itasomwa, Mnyika
alisema kwa sasa hawezi kueleza serikali watakachofanya. “Tutachukua hatua za
ziada isisomwe…nitashauriana na wabunge wengine wa Ukawa bungeni kushauriana ni
nini cha kuwafanya ili kuwe na uwajibikaji wa pamoja,” alisema Mnyika.
Kuhusu
ni hatua gani serikali ingeweza kufanya baada ya fedha za wafadhili
kutotolewa mapema, Mnyika alisema, alisema fedha za wafadhili hazipaswi kuwa
kisingizio kwa kuwa kipaumbele kingewekwa kwa kutenga asilimia 100 ya fedha za
ndani.
Mnyika alisema suala si Waziri wa Maji,
isipokuwa anayo orodha ya mawaziri wanaokwamisha mipango hiyo ya maji ambayo
ikifika wakati, atawataja wote.
Post a Comment