LIGI KUU MSIMU WA 2015/2016 SASA TIMU 16


Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuanzia msimu wa 2015/2016 itakuwa na timu 16 badala ya 14 za sasa.

Mabadiliko hayo yamepitishwa na Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyokutana jana (Mei 3 mwaka huu) jijini Dar es Salaam baada ya kupokea mapendekezo ya kuongeza idadi ya timu kutoka kwenye Kamati ya Mashindano.

Uamuzi huo umefanywa kwa lengo la kuongeza ushindani katika ligi hiyo, na kuwezesha wachezaji kupata mechi nyingi zaidi za mashindano. Kwa mabadiliko hayo maana yake ni kuwa Ligi ya msimu wa 2015/2016 itakuwa na mechi 240 wakati kwa sasa ina mechi 182.

Kuhusu idadi ya wachezaji wa kigeni kwenye VPL, Kamati ya Utendaji itafanyia uamuzi mapendekezo katika eneo hilo baada ya kwanza kupata maoni ya klabu za VPL na Ligi Daraja la Kwanza (FDL) ambazo Mei 11 mwaka huu zitakutana na Rais wa TFF, Jamal Malinzi.

Mapendekezo ya Kamati ya Mashindano ni kuwa idadi ya wachezaji wa kigeni iendelee kuwa watano kama ilivyo katika kanuni za sasa za VPL.


BONIFACE WAMBURA
OFISA HABARI NA MAWASILIANO
SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)

Post a Comment

أحدث أقدم