Wafanyakazi
wa Kampuni ya Strabag inayojenga barabara za kasi jijini Dar es Salaam,
wamerejea kazini baada ya mgomo wa siku saba.
Hayo
yamethibitishwa na Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Migodi, Nishati,
Ujenzi na Kazi nyinginezo (TAMICO), Abdulah Rukusa wakati akifanya mahojiano na
gazeti hili jijini Dar es Salaam.
Alisema
mgomo wa wafanyakazi hao, haukuwa chini ya chama hicho, ila baadhi ya
wafanyakazi waliamua kufanya mgomo baada ya kutokea vipeperushi vyenye
kuashiria suala la ubaguzi.
Aliongeza
kuwa wafanyakazi hao, ambao ni Watanzania walilalamika kuwa kuna ubaguzi
unaofanywa na kampuni hiyo kwa wafanyakazi huku wafanyakazi kutoka Kenya,
Wahindi na Wazungu wakipewa kipaumbele kuliko wao.
Alisema,
wafanyakazi hao walidai wanabaguliwa na kampuni na hawapatiwi zana za kazi,
kama wengine na hata zikitolewa, wanapewa kwa ubaguzi.
Pia,
walikuwa wakidai posho, ambazo kwa madai zinatolewa kibaguzi, vibarua hawapewi
ila wenzao wa nje wanapewa na waliamua kupeleka madai yao kwenye Tume ya
Usuluhishi na Uamuzi (CMA) na kwamba posho zilisitishwa tangu Oktoba mwaka
jana.
“Madai
hayo yalipelekwa mahakamani na posho zilisitishwa mpaka Mei 15, mwaka huu kesi
itakaposikilizwa tena,” alisema Rukusa.
Aidha,
alisema baada ya RAS, DART na Strabag kukaa waliona madai ya wafanyakazi yana
uzito na waliwasihi wafanyakazi kurejea kazini na waendelee kusubiri.
Baada
ya wafanyakazi kurejea kazini, kampuni imewateua wafanyakazi 20 kwa ajili ya
kwenda kusikiliza kesi hiyo.
“Kuna
baadhi walikuwa wanapinga kurejea kazini, lakini walirudi, ila kwa sasa
kazi inaendelea kama kawaida,” aliongeza.
Rukusa
alisema watahakikisha wafanyakazi wanapewa zana za kazi bila ubaguzi na madai
yao yanashughulikiwa kwa wakati ili kuepusha migogoro, ambayo inakwamisha
ujenzi.
إرسال تعليق