Mpira Pesa wampa urais Dalali

WANACHAMA wa Kundi la Mpira Pesa la Simba, wamefunguka kuwa, anayefaa kuwa rais wa klabu hiyo kwa miaka minne ijayo ni Hassan Dalali kwa kuwa ni mtu mwenye hekima na busara.
Dalali aliwahi kuwa mwenyekiti wa klabu hiyo kabla ya Ismail Aden Rage lakini alipigwa zengwe katika uchaguzi uliopita kutokana na kukosa cheti cha kidato cha nne na sasa yupo ‘skuli’ anaendelea kula kitabu apate cheti hicho.
Simba inatarajia kufanya uchaguzi mkuu Juni 29, mwaka huu kwa nafasi mbalimbali za urais, makamu wa wa rais na wajumbe wa kamati ya utendaji watakaoiongoza klabu hiyo kwa kipindi cha miaka minne.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Mwenyekiti wa Tawi la Mpira Pesa lililopo Magomeni jijini Dar, Ustadhi Masud, alisema wanamchukulia Dalali kama Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kutokana na kufanikiwa kuondoa makundi ndani ya klabu hiyo tangu alipopata madaraka mwaka 2006.
“Simba kwa sasa inahitaji kiongozi mwenye hekima na busara tofauti na kiongozi aliyepita Ismail Aden Rage ambaye anaonekana kujisifu yeye na kuwatukana watu, jambo hilo halikuwepo katika uongozi wa Dalali ambaye amekuwa na sifa zote za kuwa kiongozi.
“Kiongozi anayetakiwa kuongoza awe msikivu kwa kusikiliza  fikra za kila mtu mwenye uwezo na asiye na uwezo kwani Simba ni ya watu tofautitofauti, Dalali ni mtu anayefaa kuongoza tena Simba kwani tunamchukulia kama Nyerere, japokuwa uchukuaji wa fomu ni mapendekezo ya mtu binafsi, hatuwezi kumlazimisha lakini iwapo atachukua basi huyo ndiye tunayemhitaji.
“Alikuja Simba mwaka 2006 na kukuta makundi na alifanikiwa kuyaondoa. Pia alifanikiwa kutwaa ubingwa bila kufungwa na kutoa sare mbili tu, vilevile hana kashfa yoyote ya kuihujumu timu. Na kama yeye hatagombea, mtu anayetakiwa kugombea awe mwenye sifa kama zake,” alisema Masud.

Post a Comment

أحدث أقدم