Ripoti: Wawindaji halali ndiyo wanaovuna tembo

Uchunguzi huo ulibaini kuwa vinasaba vya pembe hizo vilifanana, hivyo kujenga dhana kwamba baadhi ya watu wamekuwa wakiwinda katika hifadhi hiyo mara kwa mara katika utaratibu maalumu unaotambuliwa na Serikali.PICHA|MAKTABA

Ongezeko la kasi ya ujangili nchini limedaiwa kusababishwa na vitendo vya rushwa, matumizi mabaya ya madaraka na mfumo dhaifu wa usimamizi wa sheria katika Wizara ya Maliasili na Utalii.
Kwa mujibu wa ripoti iliyopewa jina la Urasimishaji wa Ujangili wa Kitaalamu Afrika, tangu mwaka 2000 wizara hiyo imejikuta katika kashfa za rushwa na kusababisha mawaziri na watendaji wakuu kuvuliwa nyadhifa zao.
Katika ripoti hiyo, Taasisi ya Kimarekani ya Utunzaji Wanyamapori ya Born Free USA kwa ushirikiano na Shirika la Ripoti za Kichambuzi na Takwimu la C4ADS, imeeleza pia jinsi vikundi vya waasi barani Afrika wanavyoendesha shughuli za ujangili.
Ripoti hiyo iliyozinduliwa mwezi huu nchini Kenya, inaitaja Tanzania kama kitovu cha kusafirisha pembe za ndovu katika ukanda wa Afrika Mashariki na Bandari ya Dar es Salaam imekuwa ikishindana na ile ya Mombasa katika kutumia bandari kibiashara.
Kutoka mwaka 2008 mpaka 2013, inaelezwa zaidi ya tani 20 za pembe za ndovu ama zilikamatwa zikisafirishwa kuingia au kutolewa katika Jiji la Dar es Salaam, hii ni kwa mujibu wa taarifa ya Taasisi ya C4ADS.
Ripoti hiyo inafafanua kuwa uchunguzi wa vinasaba (DNA), katika tani 11 za pembe za ndovu zilizokamatwa Taiwan, Japan na Hong Kong mwaka 2006, ilibainika kuwa pembe 1,500 zilitoka Tanzania (Selous).
Uchunguzi huo ulibaini kuwa vinasaba vya pembe hizo vilifanana, hivyo kujenga dhana kwamba baadhi ya watu wamekuwa wakiwinda katika hifadhi hiyo mara kwa mara katika utaratibu maalumu unaotambuliwa na Serikali.
“Kuna udhaifu mkubwa katika usimamizi wa uwindaji halali na wawindaji wenye vibali hawasimamiwi ipasavyo kufanya uwindaji kwa taratibu zilizowekwa kisheria. Hivyo hutumia nafasi hiyo kufanya vitendo vya ujangili,” inasema sehemu ya ripoti hiyo.
Serikali yakanusha
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Wanyamapori, Paul Sarakikya alikanusha madai hayo akisema siyo kweli kwamba wawindaji halali huachwa bila usimamizi, bali wana mifumo ya kusimamia shughuli hiyo.
“Sikubaliani na ripoti hiyo, tumeshaongea sana juu ya suala hili, Rais alishalizungumzia na waziri pia. Ufafanuzi ndio huo, hamna ukweli wowote katika ripoti hiyo,” alisisitiza Sarakikya.
Salakikya alisema idadi ya tembo nchini inazidi kuongezeka katika hifadhi tofauti na upungufu unaoelezwa katika ripoti hiyo.
Mkurugenzi huyo alihoji kuwa kama hakuna usimamizi madhubuti katika uwindaji halali, wamewezaje kusimamia uwindaji miaka yote mpaka idadi ya tembo inaongezeka, baada ya upungufu uliokuwepo miaka ya nyuma.
Wakati Sarakikya akisema tembo wanaongezeka, ripoti hiyo inaeleza kuwa idadi ya tembo katika hifadhi za Selous na Mikumi kwa mwaka 1976, ilikuwa ni 109,419 lakini kufikia mwaka 2009, idadi hiyo ilishuka hadi kufikia tembo 38,975.
Nchi zilizoathirika zaidi na ujangili barani Afrika, zinatajwa kuwa ni Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Cameroon, Msumbiji, Kenya, Zimbabwe na Tanzania ambayo pia inatajwa kuwa kitovu cha usafirishaji wa pembe za ndovu.
Idadi ya tembo waliosalia
Na kwa utafiti uliofanywa na Taasisi ya Frankfurt Zoological Society mwishoni mwa mwaka 2013, ripoti hiyo inaeleza kuwa ni tembo 13,084 wanaokadiriwa kusalia katika hifadhi, sawa na upungufu wa asilimia 66 katika kipindi cha miaka minne tangu 2009.
Hii imefafanuliwa kuwa zaidi ya tembo 25,000 waliuawa katika Hifadhi ya Selous ndani ya miaka minne pekee. Pia, ripoti hiyo inabainisha upungufu wa tembo katika hifadhi ya Ruaha-Rungwa kutoka tembo 35,461 mpaka tembo 20,090 sawa na upungufu wa asilimia 36.5 kuanzia mwaka 1990 mpaka sasa.

Post a Comment

أحدث أقدم