Serikali yaagiza COSOTA, TRA kukutana kulinda maslahi ya wasanii .




SERIKALI  imetoa maagizo kwa Chama Cha Hatimiliki Tanzania (COSOTA) kukutana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuangalia namna ya kuboresha stika zinazobandikwa katika kazi za wasanii.
 Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi, Mwigulu Nchemba alitoa kauli hiyo bungeni jana ambapo alitaka COSOTA na TRA kukutana ndani ya siku tano kuangalia namna ya kuboresha stika zinazobandikwa katika kazi za wasanii  ili badala ya kutumika kukusanya ushuru peke yake zitumike pia kulinda kazi za wasanii hao .
Pia alisema kwa kazi zote zitakazokuwa zinauzwa bila stika au  kwa kazi zitakazobandikwa stika zisizo halali wachukuliwe hatua mara moja.
Mwigulu alikuwa akijibu swali la  nyongeza la Mbunge wa Viti Maalum, Martha Mlata (CCM) ambaye alisema  stika ambazo zinatumika kulinda kazi  za wasanii hazisaidii badala yake zinawasaidia TRA peke yake kukusanya mapato
Aidha akiuliza swali la nyongeza, Mbunge wa Kasulu, Felix Mkosamali (NCCR-Mageuzi) alisema kumekuwa na makampuni ambayo yananyonya wasanii na serikali ina kauli gani katika hilo.
“makampuni mengine bado yananyonya wasanii licha ya serikali kuanziish utamaduni wa kuweka stempu kwenye kazi za wasanii lakini kazi zisizo na stempu bado zinahujumiwa kwa nini msijifunze kutoka Nchini Uganda ambapo wamefanikiwa katika kulinda kazi za wasanii? ” alihoji  Mkosamali.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Habari, vijana utamaduni na Michezo Juma Nkamia alisema kuna taarifa kuwa kazi za wasanii zinazgaa mitaani na serikali inachukua hatua kwa kushirikiana na wadau katika kuondoa kazi hizo.
“Kama Uganda wamefanikiwa katika hili tuko tayari kwenda kujifunza” alisema
Awali katika swali la msingi la Mbunge wa Kasulu Mjini, Agripina Buyogera (NCCR-Mageuzi)  alitaka kujua lini Serikali itawatambua wasanii kisheria ili kulinda kazi zao ikiwemo kutunga sheria nzuri nzuri kulinda haki za wasanii.
Akijibu swali hilo, Nkamia alisema Serikali inawatambua wasanii wa filamu na muziki pamoja na tasinia nyingine za sekta ya filamu.
Aidha, alisema Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki ipo katika hatua za maamuzi Serikalini.
Source: Sifa Lubasi, habariLeo,BungeniDodoma

Post a Comment

أحدث أقدم