Kongamano
hilo la siku mbili lenye kauli mbiu ya ‘Utafiti wa Afya, Mafunzo na Ubunifu kwa
Maendeleo Endelevu’, limeandaliwa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi
Muhimbili (Muhas).
Kaimu
Mkuu wa chuo hicho, Profesa Eligius Lyamuya, alisema juzi Dar es Salaam kwamba
utafiti huo utatolewa mbele ya wanasayansi washiriki 350 toka nchi tisa
duniani, ambao watatumia kongamano hilo kubadilishana ujuzi na uzoefu katika
ufanyaji utafiti.
Mada
zaidi 138, zinatarajiwa kuwasilishwa katika kongamano hilo, ambapo kati ya hizo
mada 122 zitawasilishwa kwa njia ya mdomo, ikiwemo ya utafiti wa chanjo ya
Ukimwi pamoja na magonjwa yasiyoambukiza.
Mwaka
jana Kiongozi wa Jopo la
Wataalamu wa Muhas wanaofanya utafiti huo, Profesa Muhammad Bakari, alitoa
ufafanuzi kuhusu majaribio ya chanjo hiyo, akisema bado walikuwa wakiendelea
kuifanyia utafiti zaidi.
Profesa
Bakari alikaririwa akisema majaribio ya chanjo hiyo yaliyofanyika nchini mwaka
2007 mpaka 2010 na 2008 mpaka 2012, yalionyesha mafanikio mazuri, ingawa
hayakufikia hatua ya kupatikana kwa chanjo kamili.
Kwa
mujibu wa Profesa Bakari majaribio hayo yalithibitisha kuwa chanjo ya DNA –
MVA, ilikuwa salama na yenye uwezo wa kuufanya mwili utengeneze kinga dhidi ya
virusi vya Ukimwi (VVU).
Pamoja
na matokeo hayo ya kutia moyo, baada ya kuanza kufanya utafiti, jopo la
madaktari bado liliendelea na utafiti zaidi ulioanza 2008 hadi 2012 ili kupata
chanjo.
“Hatukuishia
hapo, utafiti wa pili (TAMOVAC-01), ulifanyika kati ya 2008 na 2012.
Utafiti huu ulijumuisha pia nchi jirani ya Msumbiji,” alisema.
Alisema
utafiti wa awali ambao uliojulikana kama HIVIS-03, ulihusisha askari 60 ambao
walifuatiliwa kwa karibu wakati wote wa utafiti, ili kuhakiki usalama wa chanjo
na uwezo wa chanjo kutengeneza vichocheo vya kinga dhidi ya VVU.
Profesa
Lyamuya alisema mada nyingine ni pamoja na maendeleo katika kushughulikia
Malengo ya Maendeleo ya Milenia katika suala la afya, utafiti wa mifumo ya afya
na nyinginezo.
“Kongamano
hilo litatumika kuhamasisha matokeo ya utafiti, ili yatumike na watekelezaji,
wadau wa afya, watoa huduma wa afya na wengine wanaofanya kazi katika maeneo
husika ya kitaaluma,” alisema Profesa Lyamuya.
Wataalamu
hao mbali na kutumia kongamano hilo kubadilishana mawazo na ujuzi kuhusu
utafiti mbalimbali, pia wataweka mikakati mbalimbali kwa wadau wa ndani na nje
ya nchi, kuhusu kutumia utafiti mbalimbali wa afya kuboresha utoaji huduma za
afya, ikiwemo kuwa na vifaa madhubuti.
Kongamano
hilo ni la pili kufanyika nchini na kuendeshwa na chuo hicho, ambapo mwaka jana
makala za kisayansi 144, ziliwasilishwa na kusaidia utoaji huduma za afya
pamoja na kutunga sera kukabiliana na changamoto za kiafya.
إرسال تعليق