Straika Mrundi wa Simba akimbilia Ulaya

HARAKATI za Simba za kutaka kuimarisha kikosi chake kwa ajili ya msimu ujao wa ligi kuu kwa kusajili baadhi ya nyota wa kimataifa zimeendelea kugonga mwamba baada ya hivi karibuni mchezaji mwingine raia wa Burundi, Steve Nzingamasabo, kuikacha timu hiyo na kutimkia Ulaya.
Simba ilikuwa katika harakati za kutaka kumsajili Zingamasabo ili kukiongezea nguvu kikosi hicho ambacho kimemaliza michuano ya ligi kuu katika nafasi ya nne.
Habari za uhakika kutoka ndani ya Simba zimedai kuwa mchezaji huyo alikuwa katika nafasi nzuri ya kusajiliwa na klabu hiyo lakini hivi karibuni alipata nafasi ya kwenda kufanya majaribio ya kucheza soka la kulipwa Ulaya na  ameamua kuachana na mpango huo wa kutua Msimbazi.
Imedaiwa kuwa, hali hiyo imewasononesha viongozi wa Simba na hivi sasa wameamua kusitisha harakati zote za usajili mpaka hapo uchaguzi mkuu wa klabu hiyo utakapomalizika.
“Zingamasabo atakuwa ni mchezaji wa pili kuingia mitini kwani wa kwanza alikuwa ni Amissi Cedric ambaye pia ni raia wa Burundi ambaye naye ametimkia Ulaya kwa ajili ya kufanya majaribio.
“Kutokana na hali hiyo kwa sasa mambo yote ya usajili yamesimama mpaka hapo uchaguzi mkuu utakapomalizika,” kilisema chanzo hicho cha habari.
Harakati hizo za kuwasajili wachezaji hao zilianza hivi karibuni baada ya viongozi wa Simba kuwaona wakati wakiitumikia timu ya taifa ya Burundi ilipopambana na Taifa Stars katika mchezo wa kirafiki uliofanyika jijini Dar es Salaam kwenye Uwanja wa Taifa.
Katika mechi hiyo, Taifa Stars ilitandikwa mabao 3-0.

Post a Comment

أحدث أقدم