TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Mei 9, 2014
RCL YAANZA KUTIMUA VUMBI KATIKA VITUO VITATU
Michuano
ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) inayoshirikisha timu 27 inaanza
kutimua vumbi kesho (Mei 10 mwaka huu) katika vituo vitatu vya Morogoro,
Mbeya na Shinyanga kwa mechi mbili kila siku.
+++++++++++++++++++
SAHIHISHO:
Kutokana na marekebisho yanayofanyika
katika Uwanja wa Sokoine kwa ajili ya ukaguzi wa CAF. Mechi za RCL za
kituo cha Mbeya sasa zitachezwa kwenye Uwanja wa CCM Vwawa uliopo Mbozi
mkoani Mbeya.
+++++++++++++++++++
Kundi A ambalo mechi zake zinachezwa
Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro, African Sports ya Tanga itacheza na
Kiluvya United FC ya Pwani saa 8 mchana wakati saa 10 jioni ni Mji Mkuu
FC (CDA) ya Dodoma dhidi ya Pachoto Shooting Stars ya Mtwara.
Jumapili (Mei 11 mwaka huu) katika kundi
hilo kutakuwa na mechi kati ya Bulyanhulu FC (Shinyanga) na Kariakoo SC
(Lindi) itakayoanza saa 8 mchana wakati saa 10 jioni ni Navy FC (Dar es
Salaam) na Abajalo FC pia ya Dar es Salaam.
Kundi B katika Uwanja wa Kumbukumbu ya
Sokoine jijini Mbeya litaanza ligi kwa mechi kati ya Ujenzi (Rukwa) na
Volcano FC (Morogoro) saa 8 mchana wakati saa 10 jioni ni AFC ya Arusha
na Panone FC ya Kilimanjaro.
Mei 11 mwaka huu saa 8 mchana ni Mpanda
United ya Katavi na Magereza ya Iringa wakati Tanzanite (Manyara) na
Njombe Mji (Njombe) zenyewe zitaumana kuanzia saa 10 jioni.
Simiyu United ya Simiyu na Mvuvumwa FC
(Kigoma) ndizo zitakazoanza kucheza saa 8 mchana katika kundi C
linalotumia Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga. Saa 10 jioni ni mechi
kati ya Wenda FC ya Mbeya na mabingwa wa Mkoa wa Kagera, Eleven Stars
FC.
Jumapili (Mei 11 mwaka huu), mechi za
kundi hilo zitakuwa Singida United (Singida) na Mbao FC ya Mwanza
kuanzia saa 8 mchana wakati jioni ni pambano kati ya mabingwa wa Mkoa wa
Mara, JKT Rwamkoma FC na Geita Veterans FC ya Geita.
Ligi hiyo itamalizika Juni 2 mwaka huu
ambapo timu itakayoongoza kila kundi itapanda daraja kucheza Ligi Daraja
la Kwanza (FDL) msimu wa 2014/2015.
MAKOCHA NGORONGORO HEROES, EAGLES KUTETA
Makocha wa timu za Tanzania (Ngorongoro
Heroes), John Simkoko na Nigeria (Flying Eagles), Manu Garba wanakutana
na waandishi wa habari kuzungumzia mikakati yao kwa ajili ya mechi ya
Jumapili.
Mkutano huo utafanyika kesho (Mei 10
mwaka huu) kwenye ukumbi wa mikutano wa Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) kuanzia saa 5 kamili asubuhi.
Mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya pili
ya michuano ya Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 20 itafanyika
Jumapili (Mei 11 mwaka huu) saa 10 kamili jioni katika Uwanja wa Taifa,
Dar es Salaam.
Fainali hizo za 19 za Afrika zitafanyika
mwakani nchini Senegal zikishirikisha timu saba zitakazofuzu kwenye
mechi za mchujo, na Senegal wanaoingia moja kwa moja kutokana na kuwa
wenyeji.
Wakati Ngorongoro Heroes leo (Mei 9
mwaka huu) saa 10 jioni itafanya mazoezi yake Uwanja wa Azam uliopo
Chamazi, Flying Eagles yenyewe muda huo huo itafanya mazoezi Uwanja wa
Kumbukumbu ya Karume.
Viingilio katika mechi hiyo ni sh. 2,000
kwa sehemu zote wakati upande wa VIP itakuwa sh. 5,000. Tiketi zitauzwa
uwanjani siku ya mechi katika magari maalumu.
BONIFACE WAMBURA
OFISA HABARI NA MAWASILIANO
SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)

إرسال تعليق