AWALI ya yote, napenda kuchukua fursa hii
adhimu kuwapongeza Watanzania wote kwa kusherekea Jubilee ya Dhahabu
kutimiza Miaka 50 ya uhai wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Huu ni wasaa muhimu kwetu sote kama taifa
kutumia kikamilifu mrejesho wa maamuzi tuliyofanya huko nyuma kama
hazina ghafi. Mrejesho ukihandisiwa ndani ya vinu vya bongo zetu, waweza
kugeuka kuwa daraja la kutuwezesha kuvuka ng’ambo ya pili tayari kwa
safari ya miaka 50 mingine!
Naomba pia kutumia nafasi hii kumpongeza
Rais Jakaya Kikwete kufanikisha sherehe hizi. Pamoja na mambo mengine
mazuri, binafsi nimeguswa sana na hatua yake ya kumtunuku Jaji Joseph
Sinde Warioba Nishani ya Miaka 50 ya Muungano.
Hatua hii ni ya kishujaa, iliyohitaji
kujiuliza mara mbili mbili kabla ya kufanya uamuzi. Na kwa hakika
kabisa, hatua hiyo itapunguza kwa kiasi kikubwa mtazamo hasi ulioanza
kujengeka miongoni mwa Watanzania walio wengi.
Idadi kubwa ya wingu la Watanzania
waliokoma kufikiri kwa akili zao wenyewe, huku wakiweka rehani maamuzi
ya hatima ya maisha yao kama taifa kuhandisiwa na kundi la watu wachache
wenye ajenda za siri kufikiri, walikuwa tayari wameingizwa ndani ya
mkondo wa uasi wa kimfumo dhidi ya mtazamo sahihi wa Mzee Warioba!
Mwelekeo usio sahihi kifikra,
uliofinyangwa kupitia propaganda ndani ya ukanda wa kisiasa zilizomchora
Jaji Warioba kama kiongozi msaliti wa Muungano, zilikuwa tayari
zimetengeneza ombwe ambalo lingekuwa ni vigumu kuliziba.
Hapa nina maana kwamba Mzee huyu
aliyejitolea kusimamia kwa uaminifu mkubwa mchakato wa kupata Rasimu
bora kupitia Tume ya kukusanya maoni ya Katiba, angehetimisha uhai wake
akiwa na historia yenye taswira feki ya usaliti dhidi ya Muungano. Na
huo ndio ungekuwa wa urithi wa taswira poromoko kwa vizazi vijavyo!
Hata hivyo, Nishani hiyo muhimu, itakuwa
imebeba dhima stahiki kwa Jaji Warioba, na hata kwa Watanzania wenye
mapenzi mema, iwapo tu wewe binafsi kama Rais na Amiri Jeshi Mkuu
utaamua kufanya maamuzi magumu, lakini sahihi, kwa kuchukua hatua za
kuyarekebisha makosa ya kiuteuzi yaliyofanyika huko nyuma.
Moja ya hatua inayotakiwa kufanyika kwa
sasa, ni kuamua kuwaondoa wanasiasa ndani ya mchakato huu na kisha
kuteua Bunge jipya lenye kusheheni Watanzania wenye uchungu na taifa
hili.
Uamuzi huo kwa fikra za haraka, waweza
kuonekana kana kwamba utachukua gharama kubwa, na pia kukudhalilisha na
kukufanya uonekane kama kiongozi usiye na msimamo.
NI sawa gharama ipo. Lakini kwa upembuzi
yakinifu wenye kuutathimini mchakato huu kwa hadhi stahiki, gharama ya
kuendelea na mchakato wa kupata Katiba ndani ya mazingira haya
yanayoongozwa na maono mafupi ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, kwa
hakika, hayatatupatia Katiba bora yenye kujibu matatizo ya Watanzania.
Matokeo ni haya. Wewe binafsi (Rais
Kikwete) utakuwa umeacha historia itakayoendelea kukusuta kila siku.
Historia hiyo itakayokugharimu, itakwenda sambamba na maumivu makubwa
yatakayotokana na vilio vya Watanzania baada ya kuamka kutoka usingizini
mwao na kugundua kuwa kumbe mchakato wa kupata Katiba mpya uliasisiwa
kighiliba-ghiliba!
Na wewe binafsi (Rais Kikwete) utajikuta
ukiitafuta fursa ya kuikarabati historia uliyojitengenezea kwa uamuzi
wako uliokosa uzalendo kwa maslahi mapana ya taifa dhidi ya yale ya
Chama chako, lakini fursa hiyo itakuwa imepita milele, na wakati huo huo
kumbukumbu za mchakato huo itakuwa imeandikwa kwenye ukuta wa bongo za
chuma kama sehemu ya historia yako binafsi isiyoweza kufutika.
Kwa heshima na taadhima, nakuomba uchukua
uamuzi huo sasa, kwa kuwa gharama yake ni ndogo sana ikilinganishwa na
gharama ya kuendelea na mchakato huu uliopoteza mwelekeo!
Wale wote waliobahatika kusoma makala
yangu ya wiki iliyopita kwenye Raia Mwema, Toleo Maalumu la Muungano,
watakumbuka kwamba dhima ya makala yale ilikuwa ni kujaribu kujenga
mtazamo ulio sahihi kifalsafa juu ya kutumia histori iliyohifadhi makosa
ma mafanikio yetu kama taifa, kama mtaji wa kuendeleza ujenzi wa taifa
kubwa.
Kwamba kuwajadili waasisi wetu wa
Muungano kwa mazuri yao na udhifu wao, ni suala lisiloepukika kwa kuwa
ni mchakato muhimu utakaoweza kutusaidia katika kuvuna tunu maridhawa
kwa ajili ya kusheheneza Katiba yetu mpya. Taifa lisilojifunza kupitia
makosa yake, hilo ni taifa mfu!
Makala hayo yalimeibua mjadala miongoni
mwa kada mbalimbali. Mmoja wa wanazuoni waliotoa mrejesho kwangum ni
Jaji Warioba. Baada kusoma makala tajwa hiyo ya Toleo Maalumu la Jubilee
ya Miaka 50 ya Muungano, iliyobeba kichwa cha habari kisemacho:
“Tuwaenzi Waasisi wa Muungano kwa kujadili udhaifu na ubora wao,”
kupitia ujumbe wa simu yake ya mkononi, alileta mrejesho huu; namnukuu:
“Kinachoendelea bungeni ni walio wengi
kutaka kupitisha mambo yao wakati walio wachache wakizuia hali hiyo
isitokee, huku Rasimu nzima ikiwa imeachwa pembeni.” (Jaji Warioba)
Huo ndio ukweli mchungu wenye kuleta kero
na simanzi. Kwamba Bunge Maalumu la Katiba limekosa muafaka wenye maono
ya kitaifa. Na kwa hakika, halina udhu wa kuwepo pale Dodoma.
Kwa sababu, kwa mujibu wa Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba, dhima ya Bunge ni kujadili na kurekebisha, na hata
kuboresha Rasimu ya Katiba iliyopo. Hawa, hawana uhuru usio kikomo.
Kwa staili ya mjadala unaoendelea, kwa
hakika, ni kama kundi fulani la wahuni walioamua kuasi majukumu muhimu
waliyoitiwa, na kuanza kujadili mambo yao ya maisha.
Watu kama hawa, Baba wa Taifa, Mwalimu
Julius Nyerere angewafananisha na mtu aliyesaliti wajibu wake adhimu wa
kuokoa maisha ya wanakijiji waliokumbwa na baa la njaa.
Naam, angesisitiza akisema, ni sawa na
mtu aliyepewa na wanakijiji chakula kidogo kilichosalia ili baada ya
kula na kushiba, aondoke kwa nguvu ya chakula hicho kwenda nchi za mbali
kuhemea.
Iwapo mtu wa namna hiyo, aliyefadhiliwa
kiasi hicho akiamua kutumia fursa hiyo kujinufaisha binafsi, hawezi
kupewa jina lenye kuweza kumpatia taswira sahihi zaidi ya jina la
msaliti, tena muuaji!
Kitendo cha wanasiasa kutumia wingi wao
ndani ya Bunge Maalumu la Katiba kupora maoni ya wananchi, ni usaliti na
hujuma ya hali ya juu. Huo ni usaliti wa kisiasa unaokwenda sambamba na
kufisidi rasilimali ndogo ya walalahoi kwa ajili ya kutengeneza Katiba
mpya feki.
Niseme hivi; moja ya makosa yaliyofanyika
wakati wa kuijenga misingi ya utaifa wetu, ni kukosekana kwa muafaka wa
kitaifa jumuhishi juu ya aina ya Muungano utakaokuwa na tija.
Mungano utakaosaidia jamii ya washirika
wa Muungano kuvuna rasilimali zao kwa uhuru na hivyo kujiletea maendeleo
ya haraka. Muafaka wa kitaifa utakaorutubusha uzalendo kwa taifa lao.
Wachambuzi wengi wa historia ya Muungano
wetu huu, wamebainisha kwamba pamoja na kusukumwa na mambo mengine, moja
ya msukumo uliopelekea Muungano wetu huu kufanyika katika mazingira ya
udharura-dharua, ni hofu ya Mwalimu Nyerere ya kwamba visiwa vya
Zanzibar vingeweza kutwaliwa na Jamhuri ya Kisovieti.
Lakini pia kulikuwa na hofu ya Usultani.
Baadhi ya wachambuzi makini, wanadai kwamba Mwalimu Nyerere aliwahi
kumtishia Sheikh Abeid Amani Karume kwamba iwapo hatakubaliana na
Muungano, basi atambue kwamba yeye atawaondoa wanajeshi 300 waliokuwa
wakimpatia ulinzi. Hivyo kwa taathira, ni vitisho.
Kwa maana nyingine, Muungano huu
uliasisiwa katika mazingira ya hofu na wasiwasi. Wananchi hawakuwa na
fursa ya kutafakari kwa kina ili kufanya uamuzi sahihi dhidi ya taifa
lao. Je; nini kilifua?
Kwa bahati mbaya, hata baada ya
kufanikisha Muungano huo ulioanza na manunguniko, fursa ya kurekebisha
makosa yaliyotokana na uamuzi wa haraka, haikupatikana hadi vifo vya
waasisi wote wawili. Kwa nini? Vitisho viliendelea kutumika kama ngao ya
kubaka fikra huru. Ukimya na utulivu uliotokana na woga na hofu,
ukatafsirika kama utulivu na amani!
Kuna tetesi kwamba kabla ya kifo cha Mzee
Karume, aliwahi kukereheshwa na mwenendo wa Muungano. Kereheko hilo
lilipelekea kutamka kuhusu maswaibu ya Muungano; akisema: “Kama koti
likikubana, si unalivua?” Je; angelivua? Binafsi sijui. Ila lilimbana,
na hadi anafariki lilikuwa halitoshi. Kwa bahati nzuri au mbaya;
vijukuu, virembwe na virembwekeze, wameendeleza kilio ya kwamba koti
hilo haliwatoshi!
Kwa mukutadha huo, hoja yaweza kuwa ni
hii. Je; twawezaje kuinuka kama taifa na wakati huo huo tukiepuka
kurudia makosa ya waasisi wetu ya kung’ang’anizana makoti yanayobana?
Je; mazingira ya mchakato wa Katiba
hayaakisi ukweli ya kwamba sote kama taifa, hatujanufaika na makosa ya
waasisi wetu; ya kwamba kuna kila dalili na kuendelea na koti lile lile,
lililowekwa viraka ving’avu? Hebu tujitathimini.
Kauli za viongozi wetu zinazoendelea kwa
sasa; kwamba Muungano wa Serikali tatu utasababisha Jeshi liasi na
kuchukua nchi, zina mwelekeo gani kama si mwelekeo ule ule uliotengeneza
misingi ya Muungano yenye matege? Ni vitisho na kutiana hofu tu!
Tumeamua kuendesha mchakato wa Muungano
kwa shinikizo la hofu ya kutengenezwa. Tumetumia mijadala iliyosheheni
hila na udanganyifu ili kukidhi maslahi yetu binafsi. Nini matokeo yake?
Maamuzi karibu yote yanayofanywa ndani ya
muktadha wa hofu, hayarutubushi fikra tunduizi; hayachipuki kupitia
mijadala huru iliyojaa mifano na takwimu za kisayansi.
Kwa maana nyingine, mwisho,
kinachozalishwa kupitia mazingira ya hofu na Katiba yenye maono mafupi
yaliyojikita katika kuziba ombwe la hofu na wasiwasi ambavyo ni zao la
propoganda tu za kisiasa.
Chanzo: Raia Mwema
إرسال تعليق