Lengo la mradi huo ulioanzishwa Januari 2012 ni kuhakikisha wajawazito
700,000 wasio na uwezo katika mikoa hiyo, wanapata uhakika wa huduma
bora za uzazi na salama kupitia mfuko huo wa bima ya afya na kuchangia
upatikanaji wa vifaa bora vya kisasa vya kuwahudumia na pia kuzikinga
familia za akinamama hao kwa kuwapatia kadi za matibabu katika kipindi
hicho.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Hamis Mdee, alisema jana kuwa mradi huo
unaotekelezwa katika mikoa ya Tanga na Mbeya, hadi Machi 31, mwaka huu
umewanufaisha wajawazito 109,184, ikiwa ni sawa na asilimia 155 ya lengo
la kuwafikia wajawazito 70,000 ifikapo Desemba mwaka huu.
Mdee alitaja mafanikio mengine ya mradi huo, uliogharimu Euro milioni
13, ambapo Euro milioni 6.6 zimetolewa na NIHF, ni akinamama zaidi ya
asilimia 60 sasa wanajifungulia katika vituo vya matibabu, ikiwa ni
kiwango cha juu cha wastani wa kitaifa ambacho ni asilimia 50.
Alisema vifo vya watoto wachanga, vimepungua kutoka vifo tisa kwa vizazi
hai 1,000 hadi kufikia vifo sita kwa kila vizazi hai 1,000.
“Haya ni mafanikio makubwa kwa sababu jinsi unavyokaribia kumaliza
tatizo, ndio unakuwa na changamoto ngumu zaidi,” alieleza Mdee.
Pia alisema kasi ya vifo vya wajawazito imepungua kutoka 170/100,000 mwaka 2011 hadi 139/100,000 mwaka 2013.
Alitaja changamoto za mradi kuwa ni upatikanaji wa dawa usioridhisha
katika vituo vya matibabu, licha ya kuwa vituo vya matibabu vina vyanzo
vya uhakika wa fedha.
إرسال تعليق