Serikali
jana ilimwaga mamilioni ya fedha kwa wanafunzi, walimu, shule, halmashauri na
mikoa iliyofanya vizuri katika elimu miongoni mwake ikiwa ni kitita cha Sh
milioni tatu kilichotolewa kwa shule 60 kila moja kwa ajili ya walimu walioleta
maendeleo.
Makamu
wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal ndiye aliyekabidhi tuzo hizo mjini hapa kwenye
kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Elimu Kitaifa.
Aidha
katika maadhimisho hayo, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kupitia kwa
Waziri wake, Dk Shukuru Kawambwa imesema inaandaa uchangiaji wa kitaifa wa
madawati kwa ajili ya kukabili uhaba wa vifaa hivyo muhimu kwa maendeleo ya
sekta ya elimu.
Katika
maadhimisho hayo ambayo shule 3,217 zilizawadiwa, ikiwa ni motisha chini ya
mikakati tisa iliyoibuliwa na Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa, Dk Bilal aliasa
shule zilizopata zawadi kuhakikisha zinaendeleza bidii zidumu kushinda.
Dk
Bilal ambaye alitaka mikoa mingine kuiga mfano wa Mkoa wa Kagera ambao ulitajwa
mara kwa mara kwa kuwa na shule zilizofanya vizuri, alitaka shule ambazo
hazikupata zawadi pia kujifunza kwa wenzao.
Tuzo
zilizotolewa na Makamu wa Rais ni kwa wanafunzi 10 bora waliofanya vizuri
katika mtihani wa taifa wa kumaliza kidato cha nne mwaka jana.
Shule
60 zilizoonesha maendeleo mazuri zimepatiwa Sh milioni tatu kwa kila shule.
Fedha hizo zimeelezwa kwamba ni mahususi kwa walimu wa shule hizo waliochangia
kuleta maendeleo.
Tuzo
zimekwenda pia kwa shule 10 zilizofanya vizuri ambazo kati yake, tano ni za
elimu ya msingi na zilizobaki ni za sekondari.
Wakati
huohuo, Halmashauri ya Mbinga, mkoani Ruvuma pamoja na Mkoa wa Tanga wamepewa
tuzo kwa kufanya vizuri kitaaluma. Wengine waliopewa tuzo ni shule 10 za
msingi na sekondari zilizoonesha maendeleo ya juu.
Katika
maadhimisho hayo, pia zawadi zilikabidhiwa kwa washindi 13 wa uandishi wa insha
ambapo washindi 10 ni uandishi wa insha za mashindano ya Afrika Mashariki.
Washindi watatu ni wa insha za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika
(SADC).
Kwa
mujibu wa Dk Kawambwa, utaratibu wa tuzo kwa wanafunzi, walimu, shule,
halmashauri na mikoa unalenga kuhamasisha wanafunzi, walimu na jamii kuongeza
bidii kuleta matokeo bora zaidi.
Akizungumzia
Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa, alisema miezi 11 tangu utekelezaji wa Mpango
huo, sekta ya elimu imepata mafanikio makubwa. Pia ufaulu wa elimu ya
msingi na elimu ya sekondari umeongezeka kutoka asilimia 31 na 43 mwaka 2012
hadi kufikia asilimia 50.6 na asilimia 58.3 mwaka jana.
Post a Comment