
Mjadala wa Bunge Maalumu la
Katiba, umeanza kuibuka upya wakati Bunge la Bajeti likienda ukingoni ambapo
Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Tanzania Bara, Mwigulu Nchemba ameibuka na hoja ya
kupinga nyongeza ya siku 60 za Bunge hilo.
Akihutubia wakazi wa Manispaa ya
Iringa na vitongoji vyake katika mkutano uliopewa jina la Ondoa Msigwa Iringa
Mjini, Mwigulu alisema atapinga kwa nguvu zake zote Bunge hilo kukutana kwa
siku nyingine 60.
Wakati Mwigulu akipinga kuendelea kwa
Bunge hilo, mjumbe wa Bunge hilo na Mbunge Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto
(Chadema), ametuma ujumbe kwa wajumbe wenzake waliojiundia kundi la Umoja wa
Katiba ya Wananchi (Ukawa), kuwa ili kumuenzi mama yake mzazi Shida Salum,
aliyefariki dunia juzi na kuzikwa jana, wawaletee Watanzania Katiba mpya.
Mwigulu, ambaye pia ni Naibu
Waziri wa Fedha, alisema sababu ya hatua hiyo ni mtazamo wake kuwa bunge hilo
likiendelea kama lilivyofanyika katika awamu ya kwanza, itakuwa sawa na kutumia
vibaya fedha za walipa kodi.
Aliahidi kumshauri Spika wa Bunge
Maalumu, Samuel Sitta, amuandikie barua Rais Jakaya Kikwete, ili avunje Bunge
hilo, endapo wajumbe wake watashindwa kutumia wiki mbili za mwanzo kujadili
mambo ya msingi katika rasimu hiyo.
Kwa mujibu wa Mwigulu, ambaye pia
ni Naibu Waziri wa Fedha, nchi imepoteza fedha nyingi katika awamu ya kwanza ya
mjadala wa Katiba katika Bunge hilo, kwani kwa zaidi ya siku 40 walikuwa
wakilumbana kuhusu kanuni na muundo wa Serikali.
Alisema kuliko kuendelea kupoteza
fedha, kwa kuwalipa wabunge wanaolumbana kwa mambo yanayojadilika, ni bora
fedha hizo zikapelekwa katika sekta zingine za maendeleo.
Akizungumzia muonekano wa Bunge
hilo uliofikia hatua za baadhi ya wajumbe kuwakashifu waasisi wa Taifa, Mwigulu
alisema: “Natamani siku moja niongoze Taifa hili, ili niwafundishe watu kuwa na
adabu.”
Alisema katika mazingira ya
kawaida inawezekana watoto wakatukanana, lakini litakuwa jambo la ukosefu wa
adabu kama mtoto atamtukana baba yake.
“Hawa watu wanaojiita Ukawa hawana
adabu, wanapaswa kufundishwa adabu, ni jambo la kushangaa wanapoachwa tu
wawatukane waasisi wa Taifa hili,” alisema.
Jana katika maziko ya Shida,
ambaye pia alikuwa mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wa kuteuliwa na Rais,
Zitto aliwataka wajumbe wenzake kumuenzi mama yake kupitia viongozi wao,
Mwenyekiti wa Kamati namba nane, Job
Ndugai na Mwakilishi wa Ukawa, Profesa Ibrahimu Lipumba.
Alitoa ujumbe huo nyumbani kwa
marehemu mama yake, mtaa wa Kisangani Mwanga, muda mfupi kabla ya kwenda
makaburi ya Rubengela mjini Kigoma ambako mwili wa Shida Salum ulizikwa.
Zitto alisema kama kweli viongozi
hao wanataka kumuenzi mama yake, wamalize tofauti zao na kulifanya Bunge
Maalumu la Katiba, kuendelea na shughuli yake ya kuwaletea Watanzania Katiba
itakayowafaa kwa muda mrefu.
Alisema kuwa mama yake alikuwa mjumbe wa Bunge hilo baada ya kuteuliwa na Rais Jakaya Kikwete,
nafasi ambayo ingempa fursa ya kuandika historia ya kuwa mmoja wa wajumbe wa
Bunge hilo, katika kuandika Katiba mpya ya Tanzania.
Hata hivyo, alisema kwa kuwa mama yake aliugua na Mwenyezi Mungu kwa
kudra zake akamuondoa katika nafasi ya kuandika historia hiyo, kilichobaki ni
viongozi na wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kufikia maridhiano na kuandika
Katiba hiyo.
Zitto alisema amejitahidi kwa kadri ya uwezo wake kumsaidia mama yake
kupata matibabu ambayo yangerudisha afya yake, na kumpa fursa ya kushiriki
katika shughuli zake za kawaida, lakini Mungu alipitisha uamuzi wake ambao
hakuna wa kumpinga.
Naye Ndugai, ambaye pia ni Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, aliyeongoza wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
kwenye maziko hayo, alisema Shida alikuwa mtetezi wa Watanzania wa hali ya
chini.
Alisema yaliyotokea ni mapenzi ya Mungu na kuitaka familia
wasihuzunike kiasi cha kupitiliza, badala yake wakae pamoja na kuweka
familia pamoja na kusonga mbele katika utekelezaji wa majukumu yao ya Taifa.
Naye Profesa Lipumba, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa CUF, alisema
kuwa Shida alisimama kuwapigania watu wenye ulemavu mchango ambao alikusudia
kuutoa kwenye Bunge Maalumu la Katiba.
Hata hivyo Lipumba alionya kuwa kama kweli watu wana nia ya kumuenzi
Shida, hawana budi kusikiliza maoni ya wananchi walio wengi katika kuipata
Katiba mpya, badala ya watu wachache kutaka kuichakachua.
Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila alisema Mkoa wa Kigoma, umekuwa
na vyama mbalimbali vya siasa vyenye wabunge lakini mama yake Zitto, alikuwa
mstari wa mbele kuwaunganisha kuwa wamoja kwa ajili ya maslahi ya Mkoa wa
Kigoma na watu wake.
Katika maziko hayo Chadema, iliwakilishwa na Mbunge wa Nyamagana, Ezekiel Wenje, ambaye alisema
kuwa Shida alikuwa kiongozi aliyesimamia
anachokiamini wakati wa vikao vya Kamati Kuu na mikutano mbalimbali ya Chadema.
Maziko hayo pia yalihudhuriwa na Naibu Waziri wa Fedha, Adam Malima,
Mwenyekiti wa NCCR – Mageuzi, James Mbatia, Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter
Serukamba (CCM), Mbunge wa Kasulu mjini, Moses Machali (NCCR-Mageuzi), Mbunge
wa Nkasi, Ally Kesi (CCM), Mbunge wa Tabora Mjini, Ismail Aden Rage (CCM),
Mbunge wa Namtumbo, Vita Kawawa (CCM).
Mkoa wa Kigoma uliwakilishwa na Mkuu wa Mkoa, Issa Machibya na
Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa, Dk Walid Aman Kabourou, ambapo Mkuu wa Mkoa alisema
kuwa amefarijika kuona mamia ya watu kutoka pande mbalimbali za nchi,
wakihudhuria maziko ya Shida jambo linaloonesha kwamba alikuwa mtu aliyeishi na
watu na kuwa msaada mkubwa kwao.
إرسال تعليق