
Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), ameiomba Mahakama
Kuu Kanda ya Dar es Salaam kutupilia
mbali ombi la Katibu wa Taasisi na Jumuiya za Kiislamu Shekhe Issa Ponda kusimamisha kesi ya uchochezi
inayomkabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro.
Katika pingamizi la DPP alilowasilisha kupitia kwa Mawakili
Waandamizi wa Serikali, Bernad Kongora na Peter Njike. DPP ameiomba
mahakama hiyo kutupilia mbali ombi hilo kwa kuwa linapoteza muda wa Mahakama.
Ponda kupitia Wakili wake Juma
Nassoro aliwasilisha ombi lililopangwa kusikilizwa na Jaji Lawrance Kaduri
akiomba Mahakama hiyo itoe amri ya
kuzuia kesi ya uchochezi inayomkabili
katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro.
Aliomba kesi hiyo isimame hadi rufaa
aliyoikata mahakamani hapo kupinga hukumu ya Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu, iliyotolewa Mei 9 mwaka jana ambayo ilimtia hatiani kwa kosa Moja la
kuingia kwa jinai katika kiwanja cha
Chang'ombe Makrasi na kuhukumiwa kifungo cha
mwaka mmoja nje.
Hata hivyo DPP aliomba Mahakama hiyo itupilie mbali ombi hilo kwa kuwa
linapoteza muda wa Mahakama pia Ponda
alishawahi kuwasilisha ombi la aina hiyo na Mahakama hiyo ilitupilia mbali.
Jaji Kaduri aliahirisha kesi hiyo hadi Juni 16 mwaka huu, kwa ajili ya
kuanza kusikiliza pingamizi hilo lililowasilishwa na DPP.
إرسال تعليق