Ni mpango wa kudhibiti Ukawa wasipewe fedha endapo wataamua kususia tena vikao vya Bunge la Katiba
Iringa. Naibu Waziri wa Fedha
na naibu katibu mkuu wa CCM-Bara, Mwigulu Nchemba amesema wajumbe wa
Bunge la Katiba linalotarajia kuanza baadaye Agosti hawatalipwa kwa
mkupuo posho zote za siku 60 ikiwa ni mkakati wa kudhibiti utoro.
Akitoa
mkakati huo wa Serikali kwenye mkutano wa CCM uliofanyika Uwanja wa
Mwembetogwa na
baadaye Mafinga wilayani Mufindi, Nchemba alisema kikundi
cha Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) hawawezi kususia kuhudhuria
vikao vya Bunge la Katiba na kulipwa posho kama wajumbe wengine.
“Tukianza
tena Bunge la Katiba, nitahakikisha ninabana matumizi na kuamuru fedha
za vikao zilipwe kwa awamu na si kwa mkupuo kama wajumbe wanavyotaka
hasa wale wa upinzani,” alisema Nchemba ambaye anasimamia sera kwenye
wizara hiyo.
Hatua ya Nchemba inatokana na kitendo cha wajumbe 190
wanaounda kutoka vyama vya upinzani na makundi maalum kuamua kutoka
ndani ya Bunge la Katiba kutokana na kutoridhishwa na mwenendo wa chombo
hicho cha kuandika katiba mpya.
Mwenyekiti wa Ukawa, Freeman
Mbowe alisema kuwa wameamua kutoka ukumbini kutokana na kutoridhishwa na
mwenendo wa Bunge hilo kuwa linajadili masuala ambayo hayakuwasilishwa
na Tume ya Jaji Joseph Warioba.
Mbowe alisema kuwa Ukawa wanapinga
hoja kujadiliwa nje ya maudhui ya Rasimu ya Katiba hiyo ikiwemo CCM
kutaka kuingiza suala la Serikali mbili wakati Tume ya Warioba ilitoa
mapendekezo ya Serikali tatu.
Nchemba alisema kama bunge hilo
likiendelea na mjadala usio na tija na mizaha, atamshauri Rais Jakaya
Kikwete kulifuta kwa kuwa litakuwa linatumia rasilimali za Watanzania
bila mafanikio yoyote.
Nchemba alisema alitarajia mijadala ya
bunge hilo ingejikita zaidi kwenye mambo ya msingi yanayowagusa wananchi
wa kada zote ikiwemo jinsi ya kudhibiti ufisadi kwa kuwa na sheria kali
dhidi ya watu hao ili kunusuru uchumi.
Alisema kipaumbele cha
Watanzania si muundo wa serikali bali ni maendeleo yao na kuwa Serikali
tatu ni gharama kubwa, fedha ambazo zingetumika kuendesha serikali hiyo
zingeelekezwa kwenye sekta za maji, afya, elimu na kuwalipa walimu.
Mwananchi.
Post a Comment