
Na Greyson Mwase, Tarime
Naibu
Waziri wa Nishati na Madini anayeshughulikia madini Stephen Masele
amekemea vikali tabia ya wamiliki wa migodi kuajiri watoto wenye umri
wa chini ya miaka 18 kwani inarudisha maendeleo ya watoto hao na kwa
jamii kwa ujumla inayowategemea
Waziri
Masele ameyasema hayo kwenye ufunguzi wa semina iliyoshirikisha
wachimbaji wadogo, madiwani, viongozi wa vijiji, wilaya, madiwani pamoja
na viongozi wa vyama vya siasa inayoendelea katika jimbo la Mwibara
wilaya ya Bunda mkoani Mara.
Waziri
Masele alisema kuwa kumekuwepo na tabia ya wamiliki wa migodi, ikiwa ni
pamoja na wazazi wenye watoto wenye umri chini ya miaka 18 kuruhusu
watoto hao kufanya kazi kwenye migodi badala ya kuwahimiza kwenda shule
na kupata elimu itakayowasaidia kutoka kwenye giza.
“Kutokuwapeleka
watoto shule na kuwahimiza kushiriki katika shughuli za madini ni
kuwaharibu kisaikolojia kwa kuwakosesha elimu kama haki yao kimsingi,
ni kosa kubwa sana.” Alisema Waziri Masele
Waziri
Masele alieleza kuwa umefika wakati wa wamiliki wa migodi pamoja na
wazazi kuwahimiza watoto kuhudhuria shule ili kuweza kuwa wataalamu wa
kutegemewa baadaye katika taifa kama marubani, wahandisi, mawaziri na
madaktari.
Aliongeza
kuwa mkakati wa Serikali ni kuhakikisha kuwa kila sekta inasimamiwa na
wataalamu ambao ni wazawa kwa kuhakikisha inalipa suala la elimu
kipaumbele kikubwa.
“Inatakiwa
pindi migodi mikubwa itakapoanzishwa wataalamu wengi kwenye migodi wawe
ni wazawa badala ya kuishia kuwa vibarua na nafasi zao kuchukuliwa na
wataalamu kutoka nje.” Alisisitiza Waziri Masele.
Waziri
Masele aliongeza kuwa ili nchi yeyote iweze kupiga hatua kimaendeleo
inahitaji wataalamu katika kada mbalimbali na kuongeza kuwa serikali ipo
tayari kutoa msaada katika kuzalisha wataalamu hususani katika sekta
za nishati na madini.
Akielezea
mikakati ya serikali katika kuimarisha sekta ya madini Waziri Masele
alieleza kuwa serikali kupitia Wizara imeanza kufufua vyama vya
uchimbaji madini ikiwa ni pamoja na kuanza kutoa ruzuku kwa wachimbaji
wadogo kwani wana mchango mkubwa sana katika pato la taifa.
Waziri
Masele alieleza kuwa serikali ilianza kutoa ruzuku na itaendelea kutoa
ruzuku kwa wachimbaji wadogo watakaothibitishwa na chama cha
wachimbaji madini kuwa wanajishughulisha na shughuli za uchimbaji
madini lengo likiwa ni kuboresha maisha yao.
Alitaja
mikakati mingine kuwa ni pamoja na kuendelea kutoa elimu ya kanuni za
uchimbaji bora na salama wa madini kwa kutumia wataalamu wake sehemu
zote zenye madini nchini.
Akielezea
kanuni za uchimbaji salama wa madini Waziri Masele aliwataka
wachimbaji wadogo kuachana na matumizi ya zebaki katika uchenjuaji
madini kwani zina athari kubwa kiafya na badala yake watumie cyanide.
Waziri
Masele alisema kuwa matumizi ya zebaki yana athari kubwa kwa mchimbaji
madini ikiwa ni pamoja na jamii inayomzunguka na hata vizazi vijavyo.
Alitaja
athari za zebaki ni pamoja na magonjwa ya kansa, pamoja na kuwa na
kuwa na vizazi vya watoto wenye ulemavu wa mtindio wa ubongo.
“
Unajua athari hizi zinaweza kuonekana hata baaada ya muda mrefu, watu
wanaweza kuathirika kwa kula viumbe kama samaki vilivyoathiriwa na
zebaki iliyotokana na maji yaliyooshea madini hayo kutiririshwa ziwani
au kwenye mito.” Alisisitiza Waziri Masele.
Waziri
Masele aliwataka wachimbaji wadogo kufuata kanuni za umiliki leseni
ili kuepuka migogoro inayoweza kujitokeza kati yao na wamiliki wa
migodi.
Waziri
Masele aliongeza kuwa kumiliki ardhi hakutoshi kumpa uhalali mmiliki wa
eneo husika kuchimba madini kwani ardhi ni eneo la juu likiwa ni pamoja
na mimea na mito na si madini yaliyopo chini yake.
Aliwataka
wamiliki wa ardhi yenye madini kuomba leseni ya uchimbaji madini ili
kuweza kuchimba madini au kuingia ubia na wenye kuhitaji maeneo yao.
إرسال تعليق