KADA WA CCM KUSOMEWA MASHITAKA KITANDANI MUHIMBILI


Jopo la mahakimu watatu, lilitoa uamuzi huo jana baada ya kukubali ombi la Wakili wa Utetezi, Majura Magafu aliyeiomba mahakama kuhamia katika hospitali hiyo, kwa kuwa mshitakiwa huyo amelazwa.
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Agosti 11 mwaka huu inatarajia kuhamia katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya kusikiliza utetezi wa kada wa CCM, Rajab Maranda anayekabiliwa na kesi ya wizi wa Sh milioni 207 za Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Maranda na wenzake wanadaiwa kuiba fedha hizo kutoka Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) kupitia BoT.

Akiwasilisha ombi hilo juzi, Wakili Magafu alidai kuwa Maranda amelazwa katika hospitali hiyo na ana tatizo la kukaa, lakini anaweza kutoa ushahidi wake akiwa amelala. Pia, aliomba mahakama itoe taarifa katika hospitali hiyo ili waandae utaratibu.

Jopo hilo likiongozwa na Hakimu Mkazi, John Utamwa lilisema Agosti 11 mwaka huu mahakama itahamia katika hospitali hiyo kwa ajili ya kusikiliza utetezi wa mshitakiwa huyo na Agosti 12 na 13, wataendelea kusikiliza kesi mahakamani.

Mbali na Maranda, washitakiwa wengine ni Farijala Hussein, Ester Komu, Bosco Kimera na Imani Mwakosya. Wote kwa pamoja wanakabiliwa na mashitaka ya kuwasilisha nyaraka za uongo, kughushi na kuiba Sh milioni 207 kutoka BoT.

Inadaiwa kuwa washitakiwa walighushi nyaraka, ambazo ni pamoja na hati za makubaliano ya kuhamishiwa deni kutoka Kampuni ya General Marketing ya India kwenda Kampuni ya Rashaz (T) ya Tanzania, ambazo walizitumia kuiba fedha hizo.

Katika hatua nyingine kesi ya wizi ya Sh bilioni sita za Benki

Kuu (BoT) kupitia Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) inayomkabili Johnson Lukaza na ndugu yake Mwesiga Lukaza inatarajia kuendelea kusikilizwa leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Jana kesi hiyo ilitajwa kwa ajili ya kuendelea kusikilizwa.

Hata hivyo, Hakimu Mkazi Gabriel Mirumbe  aliahirisha kwa kuwa jopo la mahakimu wanaosikiliza, halikukamilika.

Post a Comment

Previous Post Next Post