Kikosi hicho ambacho kimeonya dhidi ya unyanyasaji na ushawishi wa rushwa kwa waendesha pikipiki (bodaboda), kimesema mikakati ya uchunguzi na upelelezi imeimarishwa kwa lengo la kudhibiti matukio ya rushwa miongoni mwa askari wake.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Taifa, Mohamed Mpinga alisema askari hao wamekamatwa kutokana na kuimarishwa kwa usimamizi wa nidhamu na mapambano dhidi ya rushwa.
Alisema, licha ya kufanya kazi kwa weledi, upo usimamizi wa karibu kwa askari wake kwa lengo la kuepusha jeshi hilo na matukio ya aibu yakiwemo ya kujihusisha na rushwa.
"Pamoja na jitihada hizi tunaomba wananchi wote kutupa ushirikiano kupambana na hali hii hasa kwa kutoa taarifa za askari wanawaomba rushwa,” alisema Mpinga.
Alisema taarifa zitawezesha kuwashughulikia kikamilifu askari husika.
Kamanda Mpinga ameelekeza wananchi hao hususani madereva wanaoombwa rushwa na askari, kuondokana na usiri kwa kuwafichua hata baada ya kuwapatia fedha.
"Kama askari akikuomba fedha zozote ni vizuri umpatie kama unazo. Na baada ya hapo, njoo utoe taarifa kwangu nami nitakurejeshea fedha hizo,” alisisitiza Mpinga akisisitiza kwamba wanao wapelelezi wa kubaini ukweli juu ya tuhuma dhidi ya askari wao.
Akilenga kujibu malalamiko ambayo yamekuwa yakitolewa mara kwa mara na waendesha bodaboda dhidi ya baadhi ya askari wa usalama barabarani, Mpinga alisisitiza, “kikubwa hapa ni ushirikiano wa kila upande, utakaowezesha tabia hii kukoma."
Akizungumzia maboresho katika mifumo ya utendaji kazi wa kikosi hicho, Mpinga alisema yamesaidia kupunguza ajali za barabarani kuanzia Januari mwaka huu tofauti na kipindi kama hicho, mwaka jana.
Takwimu alizotoa kwa waandishi wa habari zinaonesha Januari hadi Juni kumekuwa na ajali 2,096, vifo vinne na majeruhi 2,366 wakati mwaka jana, katika kipindi kama hicho, ajali zilikuwa 11,311, vifo 1,739 na majeruhi 9,889.
Mkoa wa Dar es Salaam unaongoza kwa kuwa na ajali nyingi ambazo ni 5,052 sawa na asilimia 60.2 ya ajali zote.
Kamanda Mpinga alisema katika utekelezaji wa kupunguza ajali hizo, wameimarisha kitengo cha utoaji elimu kwa umma na kuboresha programu za luninga na redio kutoa uelewa kwa wananchi.
PICHANI: Askari trafiki wakiwa kazini katika moja ya mitaa ya Dar es Salaam.
إرسال تعليق