Washitakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo jana saa 7:30 mchana wakiwa chini ya ulinzi mkali.
Kulikuwa na magari mawili ya jeshi la Magereza, magari mawili yaliyokuwa na askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) na manne yaliyokuwa na askari zaidi ya 15 wenye silaha waliovaa nguo za kiraia.
Walisomewa mashitaka na Mawakili wa Serikali, Prosper Mwangamila, Mwanaamina Kombakono, George Barasa na Brenda Nicky mbele ya Hakimu Mkazi Hellen Riwa.
Wakili Barasa alidai katika tarehe tofauti nchini kati ya Januari mwaka jana na Juni mwaka huu, washitakiwa 16 walipanga njama za kutenda kosa la kuingiza watu nchini kwa ajili ya kufanya vitendo vya ugaidi.
Alidai katika kipindi hicho, washitakiwa walikubali kuwaingiza nchini Sadick Absaloum na Farah Omary kwa ajili ya kujihusisha na vitendo vya ugaidi.
Katika mashitaka yanayomkabili mkazi wa Kitunda, Jihad Swalehe, Wakili Nicky alidai kati ya Machi 21 mwaka jana na Juni 2 mwaka huu, Dar es Salaam, pamoja na wenzake ambao hawajafikishwa mahakamani, walipanga njama za kuwaingiza watu kwa ajili ya kufanya vitendo vya kigaidi.
Kwa mujibu wa Wakili Nicky, katika kipindi hicho, Dar es Salaam, kwa kutumia mawasiliano ya mtandao wa kijamii wa facebook, Swalehe aliwasiliana na Nero Saraiva na watu wengine akiomba malighafi, fedha na ujuzi kwa ajili ya kuweka mabomu.
Ilidaiwa aliomba ujuzi huo ili aweke mabomu nchini Kenya kwa lengo la kusababisha hofu, majeraha na vifo kwa wananchi wa nchi hiyo.
Mbali na Swalehe, washitakiwa wengine ambao ni wakazi wa Zanzibar na Dar es Salaam ni Nassoro Abdallah, Hassan Suleiman, Anthari Ahmed, Mohamed Yusuph, Abdallah Hassan, Hussein Ally, Juma Juma, Said Ally, Hamis Salum, Said Salum, Abubakari Mngodo, Salum Salum, Salum Amour, Alawi Amir, Rashid Nyange na Amir Juma.
Washitakiwa hao hawakuruhusiwa kujibu mashitaka kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo isipokuwa Mahakama Kuu.
Wakili Mwangamila alidai upelelezi wa kesi hizo haujakamilika na kuomba kesi inayowakabili watu 16 itajwe Julai 23 mwaka huu kwa kuwa wanatarajia kuwasilisha ombi maalumu.
Hakimu Riwa aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 23 mwaka huu itakapotajwa. Kwa upande wa kesi inayomkabili Swalehe, itatajwa Julai 31 mwaka huu. Washitakiwa wote walirudishwa rumande kwa kuwa mashitaka yanayowakabili hayana dhamana.
Awali katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Bulimba alisema taarifa za siri kutoka kwa raia wema zimefanikisha kukamata watu 16 wakituhumiwa kujihusisha na vitendo vinavyoashiria ugaidi ikiwemo, umwagiaji watu tindikali katika maeneo mbalimbali nchini.
Alisema watuhumiwa wanadaiwa kujihusisha na uandaaji wa vijana na kuwawezesha katika nyanja mbalimbali ikiwemo kifedha, wafanye vitendo vya uhalifu wa kitaifa na kimataifa.
Kwa mujibu wa msemaji huyo wa polisi, watu hao walikamatwa katika maeneo mbalimbali ya Tanzania Zanzibar na Bara.
"Katika jitihada za kuhakikisha kwamba nchi inaendelea kuwa ya amani na utulivu na wananchi wanaendelea kufanya kazi zao za kimaendeleo bila hofu ya kufanyiwa uhalifu, tumeendelea kukamata wahalifu wa aina mbalimbali maeneo tofauti," alisema.
Jeshi hilo kupitia kwa msemaji wake Bulimba, limeshukuru wananchi na kuomba waendelee kutoa taarifa za siri zisaidie kukamata watu wanaotuhumiwa kufanya uhalifu.
Hata hivyo, alipoulizwa kama watuhumiwa hao wana uhusiano wowote na matukio ya milipuko ya mabomu ya Arusha na Zanzibar, Bulimba hakuweka bayana zaidi ya kusema maeneo hayo ni sehemu ya Tanzania na watuhumiwa hao wamekamatwa maeneo tofauti nchini.
Pia alipoulizwa endapo watuhumiwa hao wana uhusiano wowote na vikundi vya nje vya uhalifu, bila kufafanua zaidi alisema, "naomba muelewe kwamba watuhumiwa hao wanaandaliwa kufanya uhalifu wa kitaifa na kimataifa".
إرسال تعليق