Hot:- Katiba mpya baada ya uchaguzi mkuu wa 2015

Mkutano wa Rais Kikwete na Kituo cha Demokrasia umekubaliana kwamba Katiba mpya ipatikane baada ya uchaguzi mkuu wa 2015 lakini Bunge la Katiba liendelee na vikao vyake.
Rais Jakaya Kikwete akizungumza na Wajumbe wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TDC) wakati alipokutana nao kwenye Ikulu ndogo Dodoma
Viongozi wakuu wa vyama vya Siasa vyenye wabunge vinavyounda kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) na wale wa vyama visivyokuwa na wabunge wamekutana na Rais JAKAYA KIKWETE mjini Dodoma na kukubaliana kutumika kwa Katiba ya sasa iliyotungwa mwaka 1977 katika Uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2015.
Makubaliano hayo yamefikiwa baada ya kufanya majadiliano ya kina na kubaini kuwa mchakato wa Katiba unaoendelea hivi sasa hauwezi kufikia mwisho kwa muda uliopangwa na hivyo kuamua kuendelea kwa Bunge la Katiba mpaka pale litakapotoa Katiba inayopendekezwa ambao ndiyo utakuwa mwisho wa mchakato huo kwa sasa.
Mwenyekiti wa TCD JOHN CHEYO akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma akiambatana na viongozi wa vyama vingine vya Siasa amesema iwapo mchakato huo utatakiwa kufikia mwisho ipo haja ya kusogeza mbele Uchaguzi mkuu ujao jambo ambalo limekataliwa hivyo mchakato wa kutunga Katiba utaendelea mwaka 2016 baada ya Uchaguzi Mkuu.
Katika hatua nyingine CHEYO amesema yapo marekebisho ambayo yameridhiwa kufanyika katika Katiba ya sasa ikiwemo kuweka suala la Mgombea binafsi na kutoa wito kwa vyama na wadau mbalimbali wenye marekebisho wanayotaka yawemo katika Katiba mpya kuyawasilisha mapema.
Kikao hicho kilichoketi Septemba Nane mwaka huu mjini Dodoma na kuhudhuriwa na viongozi kutoka CCM, CHADEMA, NCCR MAGEUZI, CUF na UPDP kilitarajiwa kutatua utata wa kurejea au kutorejea kwa Wajumbe wa Bunge la Katiba kutoka kundi la UKAWA waliosusia vikao hivyo ingawa Mwenyekiti wa TCD JOHN CHEYO amesema suala la UKAWA halikuwa ajenda kwenye kikao hicho

Post a Comment

أحدث أقدم