Na Benedict Liwenga, Maelezo-Dodoma.
Akiongea kwa niaba ya viongozi
wengine wa kituo hicho, Mwenyekiti wa TCD, Mhe. John Cheyo amesema kuwa
Katika mashauriano hayo yaliyochukua sura ya Kamati ya Makatibu Wakuu,
Kamati ya Wenyeviti wa Vyama vya CCM, CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi
katika hatua tofauti.
Mhe. Cheyo ameeleza kuwa kamati
zote zilitoa taarifa zao kwenye vikao vya Viongozi Wakuu wa Vyama
(Summit) ya TCD ambayo wajumbe wake ni Wenyeviti, Makamu Wenyeviti na
Makatibu Wakuu wa Vyama wanachama.
Mhe. Cheyo aliongeza kuwa katika
kutafuta maridhiano, Wenyeviti na Makatibu Wakuu wa Vyama walifanya
mashauriano na Mhe. Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete siku ya tarehe 31
Agosti mwaka huu, hivyo tarehe Nane Septemba, 2014 hapa Dodoma wakatoa
tamko lao.
“Pamoja na kazi ya msingi
inayofanywa na Bunge Maalum la Katiba, mchakato wa Katiba unaoendelea
sasa hauwezi kutupa Katiba itakayotumika katika Uchaguzi Mkuu wa 2015
kwa kuwa muda hautoshi kukamilisha mchakato na kufanya mabadiliko
yatakayohitajika ya Sheria, Kanuni na Taasisi mbalimbali
zitakazohitajika”, alisema Mhe. Cheyo.
Mhe. Cheyo aliendelea kwa kusema
kuwa, kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba mwisho wa mchakato
ni kura ya maoni itakayofanyika mwezi Aprili 2015.
“Kama itabidi kura irudiwe kwa
mujibu wa Sheria iliyotajwa, kura itarudiwa mwezi Juni au Julai 2015,
muda ambao Bunge la Jamhuri ya Muungano linatakiwa livunjwe kwa ajili ya
Uchaguzi Mkuu mwezi Oktoba 2015 na ili Katiba Mpya itumike katika
uchaguzi Mkuu utakaokuja, itabidi uhai wa Bunge na Serikali uongezwe
zaidi ya 2015, jambo ambalo hatuliungi mkono”, alisisitiza Mhe. Cheyo.
Akiongelea juu ya Tangazo la
Serikali GN Na 254, Mhe. Cheyo amesema kuwa Bunge Maalum la Katiba kwa
sasa linafanya kazi kwa mujibu wa Tangazo la Serikali (Government
Notice) Na 254 lililotolewa na Mhe. Rais Kikwete tarehe 1 Agosti, 2014.
“Tangazo hilo litatumika hadi
tarehe 4 Oktoba, 2014 ambapo Katiba inayopendekezwa inategemewa
kupatikana, Wajumbe walikubaliana hatua hii iachwe ifikiwe”, alisema
Mhe. Cheyo.
Kuhusiana na Kura ya maoni, Mhe.
Cheyo ameeleza kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba baada
ya Bunge hilo kumaliza kutunga Katiba, ingefuata hatua ya kura maoni
kuthibitisha Katiba.
“Kwa kutambua kuwa hatua ya kura
ya maoni italazimisha uchaguzi mkuu 2015 kualishwa, basi hatua hii
iailishwe, na mchakato wa Katiba uendelee baada ya Uchaguzi Mkuu wa
2015”, alisema Mhe. Cheyo.
Sambamba na hayo, Mhe. Cheyo
ameishauri Serikali kuchukua hatua za kisheria ili matayarisho kwa ajili
ya Uchaguzi wa Vijiji, Vitongoji na Mitaa, yaanze haraka iwezekanavyo
ili uchaguzi ufanyike mapema hapo mwakani.
Aidha, amegusia kuhusu
Mabadiliko ya 15 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977
akasema kuwa, kwa vile Uchaguzi Mkuu wa 2015 utafanyika kwa kutumia
Katiba ya 1977, kuna umuhimu kufanya mabadiliko kidogo (minimum reforms)
katika Katiba pamoja na sheria ya Uchaguzi yatayowezesha nchi kufanya
uchaguzi huru na wa haki.
“Tayari mambo yafuatayo
yamekubaliwa, kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi kusimamia uchaguzi, Mshindi
wa Uchaguzi wa Rais ashinde kwa zaidi ya asilimia 50% (50%+1)”, alisema
Mhe. Cheyo.
Viongozi hao Wakuu wa Vyama
wamempongeza Mhe. Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa ujasiri wake na
imani yake katika kuimarisha demokrasia nchini na kuanzisha mchakato wa
kuandika Katiba Mpya ya nchi.
“Tunampongeza kwa kukubali
kukutana na kushauriana nasi kuhusu mambo ya muhimu kwa mustakabali wa
taifa letu kwa lengo la kudumisha amani, upendo na mshikamano ili nchi
yetu iende kwenye uchaguzi ikiwa ni nchi ya kujivunia yenye amani,
mshikamano na itakayokuwa na Uchaguzi Huru na wa haki, lakini pia
tunajipongeza sisi wenyewe Wakuu wa Vyama kwa kuwa tumetoka mbali na
misimamo yetu, lakini utaifa umetufanya tukubaliane katika mambo ya
msingi wa Taifa letu”, alipongeza Mhe. Cheyo.
إرسال تعليق