Askari Polisi Amkata Vidole Vinne Mfanyakazi wake wa Ndani akimtuhumu kumwibia deki.....RPC Mwanza Ageuka Mbogo, aunda tume kubaini ukweli


JESHI la Polisi mkoani Mwanza linamshikilia askari wake WP Fatuma wa Kituo cha Polisi Igogo wilayani Nyamagana kwa kosa la kumjeruhi mtumishi wake wa ndani kwa mkumkata vidole vyake vinne vya mkono wa kulia kwa panga, akimtuhumu kumwibia Deki ya Video nyumbani kwake.

Tukio hilo la kujeruhiwa kijana Steven Magessa (18), lilitokea Oktoba 20 mwaka huu katika kijiji cha Magange Mugumu wilayani Serengeti mkoani Mara nyumbani kwao kijana huyo aliyekuwa amekimbilia huko baada ya kudaiwa kumwibia mwajili wake nyumbani eneo la Igogo.

Akizungumza na G.SENGO, kijana huyo alieleza kuwa kufanya kazi kwa askari huyo kulikuja mara baada ya askari huyo kumfuata kijijini na kuomba ridhaa ya wazazi wa kijana huyo kuambatana naye jijini Mwanza ili kumsaidia kazi za nyumbani ambapo walikubaliana malipo ya kiasi cha Sh 50,000/= kila mwezi jambo ambalo askari huyo alilikiuka na kushindwa kulitekeleza kwa muda wa miezi sita.

“Nilipoona hajanilipa mshahara wangu kwa muda wa miezi sita huku kila nikimwambia ananijia juu na kunitukana matusi basi nilimuomba ruhusa ya kwenda kijijini Oktoba 15 mwaka huu kumuona mama yangu mzazi aliyekuwa anaumwa” alisema.

Steven alieleza kuwa wakati akiwa kijijini askari huyo (Mwajili wake) alikuwa akimpigia simu kumtaka arudi Mwanza kuendelea na kazi na kudai kuwa atamlipa malimbikizo ya mshahara wake kiasi cha Sh 300,000/= zilizokuwa kama deni, Steven alikubali ombi hilo kwa kuomba atumiwe nauli na pesa kidogo ya kumwachia mama yake, jambo ambalo askari huyo alikaa kimya bila majibu.

“Siku ya Oktoba 20 mwaka huu majira ya saa 4:00 asubuhi alifika kijijini akiwa na askari watatu kwenye gari la Polisi (Difenda) wa Kituo cha Mugumu na kudai kuwa nipo chini ya ulinzi kisha kunifunga pingu, akidai kuwa nilimwibia Deki ya Video na kutoroka nyumbani kwake, walinipandisha kwenye Difenda kunipeleka kituoni “ alisema.

Kijana huyo alieleza kuwa baada ya kufikishwa kituoni Mugumu askari huyo na wenzake walianza kumuhoji huku wakimpa maneno ya vitisho. 
 

Kijana huyo alipokataa kuwa hakuiba wala kutoroka, Sajenti Fatuma aliamuru kijana huyo kuvulishwa shati alilovaa na kisha akafungwa usoni na kuombwa anyooshe mkono mezani ili apewe 'Sapraizi'.

"Sekunde chache nilihisi kitu kikali kimenipitia kwenye vidole vyangu vinne vya mkono wa kulia na kufuatiwa na maumivu makali, niliusogeza mkono wangu mdomoni kuupoza kwa kuupuliza ndipo nilipo gundua kuwa nimekatwa kabisa vidole vyangu vinne vya mkono wangu wa kulia ikibakia dole gumba tu" kijana Steven alisimulia kwa uchungu.

“Niliangua kilio kutokana na maumivu na sijui vidole vyangu hadi sasa vikowapi, askari wenzake baada ya kuona nimetokwa na damu nyingi walimshauri anipeleke hospitali ya Wilaya ya Mugumu ili nipatiwe matibabu kabla ya kuondoka kuja Mwanza,” alisisitiza.

Steven alisema baada ya kupatiwa matibabu, tulienda kupanda basi ili kuja Mwanza kwa madai kuwa amenifungulia kesi ya wizi wa Deki ya Video na tuliopofika alinipeleka kituo cha Polisi Kati Nyamagana na kuniweka Mahabusu akinituhumu wizi, lakini nilipochukuliwa maelezo nilikana tuhuma za wizi na kueleza ukweli wangu ili kupata msaada.

Taarifa zingine kutoka ndani ya jeshi la polisi  zinadai kuwa askari huyo alikusudia kufanya ukatili huo kutokana na udanganyifu ambao alifanya kwa uongozi wake akiomba kupatiwa silaha (SMG) kwa ajili ya kuitumia kwenye kazi za nje lakini lengo ikiwa ni kwenda na silaha hiyo kwa ajili ya kumkamata na kumtishia kijana huyo, jambo ambalo uongozi ulimgomea.

JESHI LA POLISI LINASEMAJE?
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza (RPC), Valentino Mlowola, jana ofisini kwake amethibitisha kuwepo kwa taarifa za tukio hilo na kueleza kuwa tayari Jeshi hilo limechukuwa hatua madhubuti, hatua ya awali ikiwa ni kumshikilia askari huyo kwa kufanya ukatili huo na kujichukulia sheria mkononi kumjeruhi kijana huyo.

Mlowola alisema pamoja na kijana huyo awali kufunguliwa jalada la kutuhumiwa kufanya kosa la wizi (Jinai) na kudaiwa kutorokea kijijini kwao, bado askari huyo alitakiwa kufuata mfumo wa kiutawala na kisheria uliopo kushughulikia suala hilo badala ya kuamua kujichukulia maamuzi ya kumwadhibu mtuhumiwa kabla ya uthibitisho wa mashitaka yaliyokuwa yamefungulia.

“Nilizipokea taarifa hizi kwa mshangao na masikitiko makubwa na zimenisitua sana. Si kitendo cha kiungwana hata kidogo kwa mtu ambaye anatakiwa kufuata taratibu za mfumo wa utawala na sheria katika utekelezaji wa kushughulikia kero na matatizo ya jamii.

"Alitakiwa kutumia busara kwani tayari alishamfungulia jalada la kumtuhumu kumwibia ikizingatiwa naye ni mzazi wa watoto watano ni lazima anaujua uchungu,”alisema.

Kamanda Mlowola alisema kuwa,  kufuatia ukatili huo kufanywa na askari wake,  ameunda timu ya kikosi cha askari kwenda  kijijini Magange wilayani Serengeti mkoani Mara ili kufanya uchunguzi wa tukio hili ikiwa ni pamoja na kufanya mahojiano na familia, wananchi wa kijiji hicho kisha Hospitali ya Wilaya ya Serengeti alipopatiwa matibabu ya awali.

“Ili tupate ukweli wa jambo hili tumeunda timu hiyo, kwani kijana Steven tumemhoji ametueleza askari Fatuma alichomfanyia na kudai hakumwibia. Lakini askri wetu pia amehojiwa, awali amedai hakufanya kitendo hicho bali wananchi ndo walimfanyia ukatili huo hivyo ni mkanganyiko lakini ukweli utapatikana tu ” alisisitiza.

Mlowola aliongeza: "Tayari tunamshikilia askari huyu na tumemfungulia jalada la uchunguzi kwa taratibu za kijeshi na ikibainika katenda kosa hilo tutamfukuza kazi na kumfikisha katika vyombo vya sheria ili kuchukuliwa hatua zaidi kulingana na kosa alilofanya, lakini pia kijana Steven naye anashikiliwa kwa tuhuma alizonazo za wizi kufuatia jalada lililopo.

“Hatuwezi kuendelea kucheka na kufumbia macho kitendo hiki maana ni jambo ambalo linamgusa kila mtu hata mimi ni mzazi ukiachana na utumishi wangu wa umma. Ntahakikisha jambo hili nalishughulikia kwa umakini na kutoa taarifa kwa umma ili pia kueleza wananchi kuwa tukio hili limefanywa na mtumishi kama mtu si Taasisi ya Jeshi la Polisi .”

Post a Comment

Previous Post Next Post