IKULU ,HAZINA, MAHAKAMA ZATINGA NUSU FAINALI SHIMIWI

Kamati ya Waamuzi wa mchezo wa kuvuta kamba ikisubiri kumkaribisha Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mbarak Abdulwakil (hayupo pichani) aliyetembelea viwanja vya Jamhuri,Morogoro mapema leo kushuhudia michezo ya kuvuta kamba.
Mwamuzi wa mchezo wa kamba Bw.Ruvu Kiwanga (kushoto) akisalimiana na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mbarak Abdulwakil alipotembelea viwanja vya Jamhuri, Morogoro mapema leo.

Na Happiness Shayo,Morogoro

Timu za kamba za Ikulu, Hazina na Mahakama zimeingia hatua ya nusu fainali kwa kishindo baada ya kuzivuta timu pinzani katika michezo ya SHIMIWI iliyofanyika uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro leo.

Michezo hiyo ya kusisimua iliyovuta mashabiki wengi ilianza majira ya saa moja asubuhi ambapo timu ya kamba ya wanawake ya Ikulu iliivuta timu ya kamba ya wanawake ya Kilimo na kuibuka mshindi kwa kuvuta mivuto yote miwili.

Mchezo wa pili ulikuwa kati ya timu ya kamba ya wanawake ya Wizara ya Ujenzi na timu ya kamba ya wanawake ya Wizara ya Uchukuzi zilizolazimishana kutoka droo kwa michezo miwili ya kwanza na hatimaye Uchukuzi kuibuka mshindi kwa mvuto mmoja baada ya kuvutana kwa mara ya tatu.

Katika mchezo mwingine timu ya kamba ya wanawake ya Wizara ya Mambo ya Ndani ililazimishana droo na timu ya wanawake ya RAS Iringa na kulazimu waamuzi kurudia mchezo huo na hatimaye RAS Iringa kuibuka mshindi kwa kuwa na pointi 1-0.

Mchezo mwingine ulichezwa kati ya timu ya kamba ya wanawake ya TAMISEMI ikiivuta timu ya wanawake ya Mahakama kwa mvuto mmoja.

Kwa upande wa timu za kamba za wanaume,Ikulu iliibuka mshindi baada ya kuivuta timu ya NFRA huku Uchukuzi ikiibuka mshindi baada ya kuivuta timu ya Afya kwa mivuto yote miwili.

Timu nyingine zilizoingia dimbani kwa upande wa timu za wanaume ni timu ya kamba ya Mahakama iliyoivuta timu ya Wizara ya Mambo ya Ndani na kuibuka na pointi 2 huku timu ya kamba ya Hazina ikiivuta timu ya kamba ya Maliasili na kuibuka na pointi 2.

Timu za kamba kwa wanawake na wanaume leo zimetoana katika hatua ya robo fainali ambapo washindi wataingia nusu fainali itakayochezwa hapo kesho.


Post a Comment

أحدث أقدم