Mkurugenzi
wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Bw. Ephraimu
Kwesigabo akitoa taarifa ya mfumuko wa bei nchini kwa mwezi Septemba, 2014 leo
jijini Dar es salaam. Kulia ni Meneja wa Takwimu za Ajira na Bei wa Ofisi hiyo
Bi. Ruth Minja.
======= ====== =======
Na. Aron Msigwa-MAELEZO.
Mfumuko wa Bei wa Taifa kwa mwezi
Septemba 2014 umepungua hadi kufikia asilimia 6.6 kutoka asilimia 6.7
iliyokuwepo mwezi Agosti kutokana na kupungua kwa bei ya bidhaa na huduma
katika maeneo mbalimbali nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari
leo jijini Dar es salaam, Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Jamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Bw. Ephraim
Kwesigabo amesema kuwa bidhaa za vyakula zikiwemo mchele, mahindi, ulezi, matunda, Sukari na vinywaji baridi zimechangia kupungua kwa mfumuko
wa bei nchini
Bidhaa nyingine zilizochangia kupungua
kwa mfumuko wa bei nchini ni Sare za shule, Simu za mkononi, runinga na viatu
huku akibainisha kuwa Fahirisi za bei kwa maana ya kipimo kinachotumika kupima
mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma zinazotumiwa na kaya nchini zimeongeka na
kufikia 149.93 kwa mwezi Septemba 2014
ikilinganishwa na 140.61 za mwezi Septemba mwaka jana.
Kwa upande wa mfumuko wa bei unaopimwa kwa kipimo cha mwezi ameeleza kuwa umeongezeka kwa asilimia 0.4 kwa mwezi Septemba 2014 ikilinganishwa na asilimia 0.1 za mwezi Agosti kutokana na kuongezeka kwa Fahirisi ya baadhi ya bidhaa zikiwemo samaki, matunda, mbogamboga, mihogo na vinywaji baridi, mkaa, mazulia na dawa za Binadamu kuwa na mchango mkubwa katika ongezeko la fahirisi.
Aidha, amesema mfumuko wa bei wa
bidhaa za vyakula nyumbani na migahawani umepungua hadi asilimia 8.3 mwezi
Septemba 2014 kutoka asilimia 8.5 za mwezi Agosti 2014 na kuongeza kuwa uwezo
wa shilingi 100 ya Tanzania katika kununua bidhaa na huduma za jamii kwa mwezi Septemba, 2014 umefikia shilingi 66 na senti 70.
Kwa upande wa mfumuko wa bei wa
Tanzania na baadhi ya nchi za Afrika Mashariki Bw. Kwesigabo amesema kuwa una mwelekeo
unaofanana, Kenya ukipungua na kufikia asilimia 6.6 kwa mwezi Septemba kutoka 8.34
za mwezi Agosti huku Uganda ikiwa na mfumuko wa bei wa asilimia 1.4 mwezi Septemba
kutoka asilimia 2.8 za mwezi Agosti.
إرسال تعليق