Mahakama ya Tanzania imedhamiria kutekeleza dira yake ya haki sawa kwa wote


1 (10)
Kaimu Mkurugenzi, Kurugenzi ya Usimamizi na Uendeshaji wa Mashauri kutoka Mahakama ya Tanzania Bw. John Kahyoza akiwaeleza waandishi wa (hawapo pichani) mikakati iliyoweka iliyowekwa na Mahakama ya Tanzania ili kutekeleza dira yake ya haki sawa kwa wote na kwa wakati kwa vitendo, kwa kuhakikisha inapunguza muda wa mashauri kukaa mahakamani, wakati wa mkutano uliofanyika leo Jijini Dar es Salaam. Kulia ni Afisa Habari wa Mahakama ya Tanzania Bi. Mary Gwera.(Picha na Hassan Silayo-Maelezo).
Na Georgina Misama-MAELEZO.
Mahakama ya Tanzania imedhamiria kutekeleza  dira yake ya haki sawa kwa wote  ili kuhakikisha inapunguza muda wa mashauri na  rufaa kukaa Mahakamani kwa muda mrefu.
Hayo yamesemwa  na  Afisa Habari wa Mahakama ya Tanzania Bi Mary Gwera wakati wa mkutano uliofanyika jana Jijini Dar es Salaam.
Akizitaja hatua zilizochukuliwa na Mahakama Bi Mary alisema, kuboresha bajeti ya kushughulikia mashauri kupitia mfuko wa mahakama toka bilioni 57 kwa mwaka 2012/13 mpaka bilioni 88 mwaka 2014/15, Idadi ya vikao vya Mahakama ya Rufani vimeongezeka kutoka 26 mwaka 2012 hadi 34 mwaka 2013/14.
Aidha, Bi Mary alisema kuwa hatua nyingine ni pamoja na kuanzisha kitengo cha Mahakama Kuu Dar es Salaam kitakachoshughulikia masuala ya utatuzi wa mashauri kwa njia ya suluhu muafaka, pia uundwaji wa kamati ya kanuni za Mahakama itakayosaidia kutunga au kurekebisha kanuni ili kuhakikisha kuwa kanuni zinazotumika Mahakamani si chanzo cha kuchelewa mashauri Mahakamami
Naye, Kaimu Mkurugenzi, Kurugenzi ya Usimamizi na Uendeshaji wa Mashauri kutoka Mahakama ya Tanzania Bw. John Kahyoza alisema kuwa Mahakama imeanza kuchukua hatua za kuimarisha ukaguzi wa shughuli za Mahakama na maadili ya watumishi kwa kuanzisha kurugenzi ya ukaguzi na maadili.
Aidha, Bw Kahyoza alivitaja viwango ambavyo kila hakimu au Jaji anatakiwa kuvitimiza kwa mwaka na muda ambao mashauri yanatakiwa kuwa Mahakamani kuwa ni Mh. Jaji wa Mahakama Kuu analenga kumaliza kesi 220, Mahakimu wa Mahakama za Wilaya na Hakimu Mkazi kesi 250 na Mahakimu wa Mahakama za mwanzo kesi 260
Mahakama Kuu inatoa rai kwa Watanzania kufika Mahakamani kwa Tarehe zinazopangwa ili kuisaidia Mahakama kuhakikisha inapunguza muda wa mashauri kukaa Mahakamani.

Post a Comment

أحدث أقدم