Miss Tanzania 2014, Sitti Mtemvu.
Na Hans MloliISHU ya madai ya udanganyifu wa umri wa Miss Tanzania 2014, Sitti Mtemvu imechukua sura mpya baada ya serikali kupitia kwa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kutoa siku saba kwa Baraza la Sanaa Tanzania (Basata) kufanya uchunguzi juu ya suala hilo.
Sitti alitangazwa mshindi wa shindano hilo lililofanyika Oktoba 11, 2014 kwenye Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar na tangu hapo kumekuwa na shutuma kuhusu udanganyifu wa umri ikidaiwa umri wake ni tofauti na ule ambao ameutaja.
Akizungumza na Championi Ijumaa jana jioni, Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Juma Nkamia, alisema serikali imelikabidhi suala hilo kwa Basata na wanatarajia kutoa tamko rasmi mara baada ya kupata majibu ya uchunguzi huo.
“Tayari tumeshalikabidhi kwa Basata na tumewapa muda wa wiki moja kisha watatupa majibu na ushauri juu ya walichokigundua, baada ya hapo sisi tutajua nini kifanyike na kutoa tamko rasmi,” alisema Nkamia.
Nyaraka ambazo zinasambazwa kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha Sitti alizaliwa Mei 31, 1989 na si Mei 31, 1991 kama ilivyoelezwa na Kamati ya Miss Tanzania iliyo chini ya mratibu wa shindano hilo, Hashim Lundenga.
Baadhi ya nyaraka hizo ni paspoti ya Sitti iliyotolewa Februari 15, 2007 ikionyesha amezaliwa 1989, pia leseni ya udereva aliyoipata huko Texas, Marekani inaonyesha mrembo huyo alizaliwa Mei, 1989.
إرسال تعليق