Tumieni namba za simu kudhibiti uendeshaji holela - UDA

Miongoni mwa mabasi ya shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) yanayofanyakazi katika maeneo mbali mbali jijini Dar es Salaam. Kila na namba za simu ili kurahisisha abiria na watumiaji wa mabasi hayo kutoa maoni juu huduma zitolewazo na mabasi ya shirika hilo.

Abiria na watumiaji wengine wa barabara Dar es Salaam wameombwa kusaidia katika kudhibiti uendeshaji holela na tabia zisizokubalika zinazofanywa na baadhi ya madereva wa mabasi ya abiria na makondakta wa Dar es Salaam kupitia namba za simu zilizochapishwa katika mabasi yote ya Kampuni ya Usafiri Dar es Salaam (UDA).

Taarifa iliyotolewa na uongozi wa UDA jana na kusainiwa na Meneja Uhusiano wa kampuni hiyo, Bw.  George Maziku, imesema utumiaji wa namba hizo utaisaidia pia kampuni kuboresha utoaji wa huduma kwa wateja wake. 

 “Tunawakumbusha wateja wetu wapendwa pamoja na watumiaji wengine wa barabara kuripoti uzembe wowote au utovu wa nidhamu utakaofanywa na madereva na makondakta wa UDA ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa dhidi yao ambazo zitasaidia kuboresha huduma zetu kwa jamii kwa ujumla.”

“Mbali na kuboresha utoaji wa huduma zetu, UDA inalenga kuwa mfano wa kuigwa kwa mabasi mengine ya abiria nchini katika uzingatiaji wa sheria, utoaji wa huduma nzuri kwa wateja na kuwa kichocheo cha kupunguza  foleni katikati ya jiji la Dar es Salaam. Hii itakuja pale ambapo wamiliki wa magari binafsi watakapoanza kutumia usafiri wa umma wenye gharama nafuu,” alisema.

Bw. Maziku alisisitiza kuwa uongozi wa UDA utachukulia kwa uzito mkubwa na kuyafanyia kazi maoni yote yakayokuwa yakitolewa kupitia namba hizo zilizotolewa ili kuondokana na dhana potofu iliyopo kuwa wamiliki na waendeshaji wa kampuni za magari ya abiria ni watu ambao hawajaelimika.

Alisema kuwa, mbali na uwepo wa namba hizo za simu, UDA itaendelea na utekelezaji wa utaratibu wake wa kutuma waratibu kupanda mabasi ya kampuni hiyo na kuripoti juu ya utendaji kazi wa madereva na makondakta wa mabasi hayo.

“UDA imelenga kuhakikisha kila mteja anapata huduma bora ambazo zinakidhi matarajio yao na wakati huohuo, zikiwa zinaendana na matakwa elekezi ya usalama barabarani,” aliongeza.

UDA ina zaidi ya mabasi 400 yanayofanya kazi, hii inaifanya kuwa kampuni kubwa zaidi ya magari ya abiria Tanzania.

Post a Comment

Previous Post Next Post