Miongoni
mwa mabasi ya shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) yanayofanyakazi
katika maeneo mbali mbali jijini Dar es Salaam. Kila na namba za simu
ili kurahisisha abiria na watumiaji wa mabasi hayo kutoa maoni juu
huduma zitolewazo na mabasi ya shirika hilo.
Abiria na watumiaji wengine wa
barabara Dar es Salaam wameombwa kusaidia katika kudhibiti uendeshaji holela na
tabia zisizokubalika zinazofanywa na baadhi ya madereva wa mabasi ya abiria na
makondakta wa Dar es Salaam kupitia namba za simu zilizochapishwa katika mabasi
yote ya Kampuni ya Usafiri Dar es Salaam (UDA).
Taarifa iliyotolewa na uongozi wa UDA jana na kusainiwa na Meneja
Uhusiano wa kampuni hiyo, Bw.
George Maziku, imesema utumiaji wa namba hizo utaisaidia pia kampuni
kuboresha utoaji wa huduma kwa wateja wake.
“Tunawakumbusha wateja wetu wapendwa pamoja na
watumiaji wengine wa barabara kuripoti uzembe wowote au utovu wa nidhamu
utakaofanywa na madereva na makondakta wa UDA ili hatua stahiki ziweze
kuchukuliwa dhidi yao ambazo zitasaidia kuboresha huduma zetu kwa jamii kwa
ujumla.”
“Mbali na kuboresha utoaji wa
huduma zetu, UDA inalenga kuwa mfano wa kuigwa kwa mabasi mengine ya abiria
nchini katika uzingatiaji wa sheria, utoaji wa huduma nzuri kwa wateja na kuwa
kichocheo cha kupunguza foleni katikati
ya jiji la Dar es Salaam. Hii itakuja pale ambapo wamiliki wa magari binafsi
watakapoanza kutumia usafiri wa umma wenye gharama nafuu,” alisema.
Bw. Maziku alisisitiza kuwa
uongozi wa UDA utachukulia kwa uzito mkubwa na kuyafanyia kazi maoni yote
yakayokuwa yakitolewa kupitia namba hizo zilizotolewa ili kuondokana na dhana
potofu iliyopo kuwa wamiliki na waendeshaji wa kampuni za magari ya abiria ni
watu ambao hawajaelimika.
Alisema kuwa, mbali na uwepo wa
namba hizo za simu, UDA itaendelea na utekelezaji wa utaratibu wake wa kutuma
waratibu kupanda mabasi ya kampuni hiyo na kuripoti juu ya utendaji kazi wa
madereva na makondakta wa mabasi hayo.
“UDA imelenga kuhakikisha kila
mteja anapata huduma bora ambazo zinakidhi matarajio yao na wakati huohuo,
zikiwa zinaendana na matakwa elekezi ya usalama barabarani,” aliongeza.
UDA ina zaidi ya mabasi 400
yanayofanya kazi, hii inaifanya kuwa kampuni kubwa zaidi ya magari ya abiria
Tanzania.
إرسال تعليق