Uhuru Kenyatta aelekea ICC kama raia ndani ya "t-shirt na jeans"

Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta amewasili jijini The Hague, Uholanzi katika Mahakama Maalum ya Kimataifa inayohusika na visa vya uhalifu kwa viongozi wa nchi zilizoridhia mkataba huo, ICC, kwa ajili ya kikao maalum kuhusu kesi inayomkabili.

Siku ya Jumatatu, Rais Kenyatta alikabidhi madaraka yake kwa muda kwa Naibu Rais, William Ruto na kusisitiza kuwa anaondoka nchini humo kama raia.
Akiwahutubia Wabunge mjini Nairobi, Kenyatta aliwaambia kuwa yuko
tayari kuhudhuria kikao maalum alichotakiwa kuhudhuria mjini Hague bila wasiwasi wowote.
Kenyatta alitakiwa na majaji wa mahakama hiyo kufika ICC tarehe 8 mwezi huu kufafanua madai a upande wa mashitaka uliodai kuwa serikali ya Kenya imekataa kushirikiana na mahakama hiyo hasa upande wa mashitaka kwa kukataa kuipatia ushahidi unaohitajika katika kesi inayomkabili kama vile rekodi zake za mawasiliano ya simu na taarifa zake za kifedha.

Mbali na hilo, Ofisi ya kiongozi wa Mashtaka Jumanne wiki hii imewaomba majaji wa Mahakama hiyo kuamua kuwa Kenya haishirikiani na Ofisi hiyo kuhusu kesi inayomkabili rais Kenyatta.

Kenyatta anakabiliwa na kesi inayomtuhumu kupanga, kuchochea na kufadhili machafuko na ghasia baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2007.

Rais Kenyatta anasema anajiamini na kwamba anajua hana hatia katika tuhuma zinazomkabili.

Alisema Kenya ni nchi huru na kwamba haitawahi kuwa chini ya mamlaka nyingine yoyote.

Vyombo kadhaa vya habari na mitandao ya kijamii imeripoti kuwa takriban wabunge mia moja walikuwa wanajiandaa kuambatana na Kenyatta kuelekea The Hague katika ishara yao ya kumuunga mkono.






Post a Comment

أحدث أقدم