Na Mwinyi Sadallah, Mwananchi
Ni kuhusu kura ya maoni ya Katiba, CUF wakidai katiba hiyo haikutokana na maoni ya wananchi.
Zanzibar: Wakati Chama cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimesema
kitafanya kampeni maalumu kuhakikisha kura ya maoni ya Katiba ya
Muungano inashinda Zanzibar, Chama cha Wananchi (CUF) kimesema
kinajipanga kufanya kampeni nzito kupinga rasimu hiyo.
Hayo yameelezwa na viongozi wa vyama hivyo hivyo walipozungumza na
gazeti hili kwa nyakati tofauti jana, baada ya Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Jakaya Kikwete na Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed
Shein, kukabidhiwa Rasimu ya mwisho ya Katiba Oktoba 8, mwaka huu.
Mkurugenzi wa Uenezi na Mawasiliano ya Umma wa CUF, Salim Abdalla
Bimani alisema wabunge wa Bunge la Katiba wameshindwa kuheshimu Rasimu
iliyotokana na maoni ya wananchi yaliyokusanywa na Tume ya Jaji Joseph
Warioba.
Alisema CUF itafanya mikutano ya hadhara katika majimbo yote Unguja
na Pemba kuwaelemisha wananchi ubaya wa rasimu hiyo na kama watapitisha
Zanzibar itapoteza hadhi yake ya kuwa nchi na Rais wa Zanzibar kukosa
mamlaka ya kugawa mipaka ya wilaya na mikoa visiwani humo.
Alisema mambo mengi yaliyotokana na maoni ya wananchi yametupwa na
wabunge wa Bunge la Katiba ikiwamo wabunge kuwekewa ukomo, wananchi kuwa
na uwezo wa kumuondoa mbunge asiyewajibika, mfumo wa Muungano wa
Serikali tatu, kufutwa kwa viti maalumu, pamoja na miiko ya uongozi
kutozingatiwa.
Bimani alisema ni vizuri kura ya maoni ikafanyika baada ya uchaguzi
mkuu 2015 kama viongozi wa vyama walivyokubaliana na Rais Jakaya
Kikwete. Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Vuai ali Vuai alisema Rasimu
ya mwisho ya Katiba ni nzuri kwa sababu imegusa makundi mbalimbali
wakiwamo watu wenye ulemavu, wavuvi, wakulima , wafugaji pamoja na haki
ya kuishi na kuwataka Watanzania kuipokea rasimu hiyo.
Alisema Katiba hiyo siyo ya CCM kama wanavyojaribu kupotosha
wapinzani ikizingatiwa vyama 16 vya siasa na makundi maalumu vimeshiriki
kikamilifu kujadili na kupitisha rasimu hiyo.
Hata hivyo alisema mambo yaliyorekebishwa katika Rasimu ya Tume ya
Mabadiliko ya Katiba na wabunge walizingatia maslahi ya Taifa na
wananchi .
Msemaji wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar Idrisa Haji Jecha alisema ZEC
inaendelea kuhakiki daftari la wapiga kura wa kudumu ikiwemo kuingiza
wapiga kura wapya na kuondoa majina ya watu waliokufa kabla ya kufanyika
kwa kura ya maoni Zanzibar.
Hata hivyo alisema mpaka sasa hawajui lini kura ya maoni itafanyika
kwavile bado hawajapokea taarifa yoyote kuhusu mchakato huo kutoka Tume
ya Taifa ya uchaguzi Tanzania (NEC).
Rasimu ya Katiba inahitaji kuugwa mkono na asilimia 50 ya Wazanzibar na kwa idadi kama hiyo Tanzania bara.
Chanzo Mwananchi
Post a Comment