Picha - Maktaba |
Na Asha Salim, Pemba
WAVUVI katika wilaya ya Micheweni wametakiwa
kuchukua tahadhari kubwa juu ya maambukizi ya ugonjwa wa Ebola hasa wanapokuwa
dago nje ya kisiwa cha Pemba.
Tahadhari hiyo imetolewa na Maofisa wa Idara ya Uvuvi, wakati
wakizungumza na wavuvi pamoja na wanajamii katika kijiji cha Shumba mjini, wilayani
humo.
Walisema miongoni mwa watu wanaotakiwa kuchukua tahadhari juu ya
maambukizi ya Ebola ni wavuvi wanaotoka na kuingia katika visiwa tofauti pamoja
na kuacha tabia ya kuchukua wageni kiholela.
Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Uvuvi, Sharif Mohamed Faki, alisema ugonjwa
wa Ebola ni hatari na kwamba hauna chanjo wala tiba.
Alisema ni vyema jamii ikafuata ushauri unaotolewa na wataalamu wa
afya pamoja na kuacha tabia ya kusalimiana kwa kupeana mikono na watu wasiowajua
wakiwa safarini.
Awali akitoa maelezo mafupi kuhusiana na njia za maambukizi ya
ugonjwa huo, Ofisa Mipango Idara ya Maendeleo ya Uvuvi, Khalfan Amour Juma,
alisema ni Ebola unaambukizwa kwa kugusa maji maji ya muathirika.
Aliwahimiza wavuvi kutokula wanyama pori hasa jamii ya kima na
popo pamoja na matunda yaliyoliwa na kuachwa na wanyama hao.
Katibu wa kamati ya bandari ya Micheweni, Hussein Rashid Hussein,
aliwataka wavuvi wenzake kuwa makini wakati wanapochukua wageni ili kujikinga
na mripuko wa ugonjwa huo.
Post a Comment