*Ataka Watanzania
wajitokeze kwa wingi Oktoba 12
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amewataka
Watanzania wajitokeze kwa wingi kushangilia mechi ya viongozi wa dini wa mkoa
wa Dar es Salaam itakayochezwa Jumapili, Oktoba 12, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa,
jijini Dar es Salaam.
Ametoa kauli hiyo leo asubuhi (Ijumaa, Oktoba 10, 2014) wakati akizungumza
na wachezaji wa timu za AMANI na MSHIKAMANO zinazoundwa na Masheikh, Maaskofu,
Maimamu na Wachungaji kutoka madhehebu mbalimbali ya mkoa wa Dar es Salaam
ambao wamepiga kambi mjini Morogoro.
“Hii
haijapata kutokea… katika hali ya kawaida mkusanyiko kama huu siyo rahisi na
katika nchi nyingine kupata mjumuiko kama huu haiwezekani,” alisema wakati
akiongea nao kwenye viwanja vya michezo vya taasisi ya Highlands Baptist
Mission iliyoko Kigurunyembe, Morogoro.
Alisema
uamuzi wa viongozi wa dini kukaa pamoja na kucheza mechi hiyo ni kutaka kuonyesha
dhamira ya kweli ya kufanya mshikamano na amani kuwa ajenda ya kudumu kwa Taifa
hili.
“Mimi
ninaamini kinachotuunganisha siyo dini bali ni kutambua kwamba sisi sote
tumeumbwa na Mungu… sisi sote ni bin-adam. Dini ni milango tu ya kutusaidia
tufike kule ambako Mwenyezi Mungu anataka tuende,” alisema.
“Ukichukulia
mfano wa wakristo, kuna madhehebu mengi. Kwa hiyo hawa wakigombana tayari ni
tatizo. Hivyo uamuzi wa kuwachanganya katika timu ni jambo zuri, ni kudumisha
umoja, amani na mshikamano,” aliongeza.
“Hii
ni hatua ya kwanza kinachofuata sasa ni kuwa na One Destiny, One People, One Nation,” akimaanisha kuwa na Lengo
Moja, Watu Wamoja na Taifa Moja. Alisema hiyo ni kama sura ya kwanza
imefunguliwa hivyo, hawana budi kuendelea mbele.
Mapema, Sheikh
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Alhad Mussa Saleem alimweleza Waziri Mkuu
kwamba timu hizo ziko kambini hapo tangu Jumatano, Mei 8, 2014. Alisema
leo baada ya mazoezi watakwenda kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Mikumi na
kurejea kambini Morogoro. Wanatarajia kurejea jijini Dar es Salaam kesho (Jumamosi)
tayari kwa pambano lao la Jumapili, Oktoba 12, 2014.
Waziri Mkuu ambaye aliwasili Morogoro
jana mchana akitokea Dodoma, alifanya ziara ya siku kwa kutembelea Chuo Kikuu cha
Sokoine na leo atatembelea Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Chuo Kikuu Huria
kukagua miradi kama hiyo.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
11410
– DAR ES SALAAM.
IJUMAA, OKTOBA 10, 2014
Post a Comment