Amri ya Mahakama yazua sintofahamu bungeni

Dodoma. Miongozo iliyoombwa na wabunge jana ilizua vurumai bungeni kiasi cha kumfanya Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Azzan Zungu kutishia kuliahirisha.
Sintofahamu hiyo ilianza baada ya Mbunge wa Kishapu (CCM), Suleiman Nchambi kuanza kuzungumzia amri iliyotolewa na Mahakama kuhusu Bunge kujadili ripoti ya IPTL.
Kelele, zomea zomea na kauli za “umechukua hela wewe” zilisikika kupitia vipaza sauti vya wabunge hao hata kabla ya mbunge huyo kujenga hoja yake.
Nchambi hakujali kelele hizo na aliwaambia waliokuwa wakizomea... “mkimaliza kuzomea nitaendelea.”
Kutokana na kelele hizo, Zungu alisimama na kuwaomba wabunge kutulia na kuvumiliana akisema kila atakayesimama kuomba mwongozo atapewa nafasi.
“Waheshimiwa wabunge oda please! Waheshimiwa wabunge Bunge linaendeshwa kwa kanuni na kila atakayesimama leo (jana) na kuomba mwongozo kiti kitampa nafasi, mwacheni aombe mwongozo wake (wabunge wakaendelea kupiga kelele). Natoa onyo la mwisho kama hamtasikiliza nitasitisha Bunge sasa hivi na mtabaki mnasema miongozo yenu canteen (kwenye mgahawa),” alisema Zungu.
Baada ya kauli ya Zungu, wabunge walitulia na Nchambi akaendelea na kusema wakili ambaye amepeleka kesi hiyo mahakamani ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema. Alisema wakati wabunge wa CCM wanataka suala hilo lijadiliwe ili Watanzania wajue nini kinaendelea, mwanasheria huyo wa Chadema amekwenda kulipinga mahakamani hivyo akaomba mwongozo wa kiti cha kwa nini suala hilo limefikia hapo na kwamba kwa nini wakili huyo asijadiliwe.
Kutokana na madai hayo, Mbunge wa Iramba Mashariki na Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu alisimama na kufafanua kuwa wakili wa IPTL na PAP ni Gabriel Mnyele wa Mpanda na kwamba ni kweli mjumbe wa Kamati Mkuu wa Chadema, Mabere Marando anafanya kazi katika kampuni aliyomo wakili huyo lakini hakuhusika kufungua kesi hiyo.
Baada ya ufafanuzi huo, Lissu aliongeza kuwa kilichotokea juzi kwa Mahakama kuzuia mjadala bungeni hakijawahi kutokea tangu Mahakama ya Tanganyika ianzishwe mwaka 1922 na kuwa kinakiuka Ibara ya 100 ya Katiba ya nchi, hivyo mjadala uendelee.
Aliyefuata alikuwa Mbunge wa Simanjiro (CCM), Christopher Ole Sendeka ambaye aliomba mwongozo akieleza kuwa Ibara ya 100 ya Katiba inalipa Bunge uhuru wa kujadili suala hilo kwa kuwa macho ya Watanzania wote yapo Dodoma na wanasubiri Bunge liungane bila mpasuko wa itikadi za kisiasa... “Wanasubiri kusikia na kupata vielelezo vya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) ili waweze kujua nini kinaendelea.”
Mbunge wa Gando (CUF), Khalifa Suleiman Khalifa aliomba mwongozo akieleza kushangaa kwa nini wabunge walikuwa na haraka na jambo hilo wakati Spika, Anne Makinda alishatoa mwongozo wa suala hilo.
“Spika alichosema jana (juzi) ndiyo ruling (uamuzi) ya Bunge kwa sababu hata mtu aende msikitini au kanisani itakuja tu,” alisema Khalifa.
- Mwananchi.

Post a Comment

Previous Post Next Post