‘Tanzania kinara kutoweka wazi nyaraka za bajeti kwa wananchi’

TANZANIA imeelezwa kuwa nchi inayoongoza kwa kutoweka bajeti zake wazi kwa wananchi na hivyo kurudisha nyuma suala zima la uwajibikaji.
Hayo yalielezwa jana Jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Haki Elimu, Godfrey Boniventure, alipokuwa anatoa ripoti iliyofanywa na shirika hilo kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Nchini Marekani (International Budget Partnership) kuhusiana na suala zima la uwekaji wazi wa nyaraka za bajeti kwa wananchi.
Boniventure, alisema katika utafiti huo uliofanyika kuanzia Novemba mwaka jana hadi Julai mwaka huu na kushirikisha jumla ya nchi 30 ulimwenguni, Tanzania imeonekana kutoweka wazi nyaraka zake za bajeti.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo ripoti za robo na nusu mwaka zitasaidia wananchi kuifuatilia Serikali kwa karibu na kuona ni mambo gani wametekeleza na yapi wangependa yapewe kipaumbele.
Alisema utoaji wa ripoti hizo pia utasaidia wabunge kuweza kukaa na wananchi wao na kujadili kwa mapana wapi kuna changamoto na kuwapa mapendekezo ya nini wangependa wafanyiwe katika bajeti ijayo.
Shirika hilo limetaka katiba pendekezwa itaje suala la uwekaji wazi wa nyaraka za bajeti kwa kuwa ni haki ya wananchi kuziona na kuzijadili.
Katika utafiti huo inaelezwa kuwa Tanzania iliwasilisha nyaraka tano kati ya nane zilizohitajika.
Ripoti ambazo zilihitajika ni pamoja na Tamko la Bajeti la awali, Mapendekezo ya Bajeti Kuu, Bajeti ya wanachi, Ripoti ya Bajeti iliyopitishwa kisheria na Ripoti za Bajeti za Robo Mwaka.
Nyingine ni Ripoti ya Bajeti za Nusu mwaka, Ripoti Bajeti ya mwisho wa mwaka na Ripoti ya Ukaguzi.

Post a Comment

Previous Post Next Post