Kuna
maswala kadha wa kadha yanayoikabili Tanzania kwa hivi sasa, miongoni
mwa mambo haya ni sakata la akaunti ya Tegeta/Escrow, mchakato wa katiba
mpya na mengine mengi. Mwandishi Nova Kambota amefanya mahojiano na
Andrew Julius Nyerere ambaye ni mtoto wa kwanza wa baba wa taifa hayati
Mwalimu Nyerere, fuatana naye katika mahojiano haya………………
SWALI;
Kuna mambo kadhaa yaliyojitokeza siku za karibuni ambayo watu wanataka
kufahamu manufaa yake kwa taifa, moja ya matukio hayo ni ziara ya Jafar
Mermo Idd Amin mtoto wa rais wa zamani wa Uganda marehemu Idd Amin
mwaka 2008, je ziara hiyo ambayo ilimkutanisha na Madaraka Nyerere
walipozuru Butiama ilikuwa na manufaa gani kwa taifa?
JIBU;
Kwa familia ya Mwalimu Nyerere na familia ya marehemu Idd Amin nadhani
ilikuwa jambo zuri kuleta upatanishi, kuhusu kama taifa lilipata faida
sijui. Aliongea Jafari kuhusu kuanzisha mfuko wa hela kuwasaidia
wanajeshi walioathirika na vita vya Kagera(wa Uganda na Tanzania), pia
nchi hizi mbili zilihitaji kupatanishwa , Jenerali Musuguri alikuwa
anaongea katika redio miezi michache iliyopita, kwamba wanajeshi wetu
walikuwa na hasira sana, kabla ya kufika Kyaka walikuwa wameshawaua watu
10,000(elfu kumi), Jenerali Musuguri yupo hapa Butiama, natamani kwenda
kumuuliza kama hao wote waliouwawa walikuwa ni maadui kwasababu hii
ilikuwa ni vita yetu ya kwanza, inawezekana makosa yalifanyika.
SWALI;
Una maoni gani kuhusiana na mwenendo wa CCM iliyoasisiwa na Mwalimu
Nyerere ambayo sasa baadhi ya viongozi wake wanatuhumiwa vikali
kujihusisha na ufisadi? Hudhani ni sababu tosha kwa watanzania kuikataa
CCM ikiwa inakiuka misingi ya kuundwa kwake?
JIBU;
CCM iliamua kujiita Chama Cha Mapinduzi kwa maana ya mapinduzi
yaliyofanyika Urusi au Uchina, kwa maana kwamba watu walio wengi wakiwa
na njaa wataleta fujo za kuiangusha serikali kama wamechochewa au hata
kama hawajachochewa. Iwapo CCM itaendeleza hayo mapinduzi wananchi
wataendelea kuichagua, inategemea tu watu wangapi bado wanaamini
inaendeleza mapinduzi, maoni yangu mimi siyo muhimu, watu waamue, na
nadhani wanaweza kugawanyika katika maamuzi.
SWALI;
Miaka ya karibuni kumekuwa na watu wanaohoji namna baba wa taifa Julius
Nyerere alivyoaga dunia, baadhi ya wanasiasa wametilia shaka mara
kadhaa kifo chake mpaka ikampelekea Madaraka Nyerere kutoa kauli, vipi
mtazamo wako kuhusu hili? Kuhoji kifo cha Nyerere kuna maslahi yoyote
kwa taifa?
JIBU;
Magige , mtoto wa Mwalimu anasema kuna chanjo moja ilikuwa wapewe
watanzania ambayo Mwalimu alikuwa ana mashaka nayo. Mwalimu alimwambia
Dr Mwakyusa kwamba yeye apewe, aijaribu halafu akiridhika ataiidhinisha
wapewe Watanzania, lakini alipopewa hiyo chanjo, Mwalimu hali yake
ilibadilika ghafla, amefariki. Niliposikia hiyo stori nilimweleza Magige
kuhusu Global 2000 Report ya Warren Christopher, inasemekana katika
miaka ya sabini viongozi wa Afrika walishauriwa na IMF
wakubali wananchi wao wachanjwe chanjo za magonjwa ili watu wapungue ili
iwe rahisi kuwasaidia; kwamba tatizo la kuwasaidia ni tatizo la
logistics tu. Inasemekana ushauri huo ulikubaliwa na viongozi wetu.
Global 2000 Report ni Top Secret ipo United Nations na hata ukiwa kule
huwezi kuipata mpaka uwe na Special Clearence. No, nilimwambia Magige
hatutapata faida yoyote tukianza kuuliza maswali kuhusu kifo cha
Mwalimu, kama kuna mtu anabisha kwamba World Health Organization inaweza
kufanya ufisadi, mtu huyo huwa anashauriwa kufanya utafiti jinsi W.H.O
ilivyoanzishwa.
SWALI;
Unazungumziaje mchakato wa kupatikana kwa katiba mpya nchini, kutokana
na matukio yanayoendelea kujitokeza kama Mzee Warioba kupigwa na hali ya
kutoelewana miongoni mwa watanzania, Je unaona wapi tumekosea? Nini
kifanyike kunusuru mchakato huu ili tupate katiba itakayolivusha taifa
letu kutoka hapa tulipo?
JIBU;
Hakuna matatizo kuhusu katiba , isipokuwa kama kuna maoni yanayoweza
kuiboresha katiba , maoni mapya ambayo siyo ya UKAWA , sasa ndiyo wakati
wa kuyatoa.
SWALI;
Unazungumziaje uongozi wa baba wa taifa hayati Mwalimu Nyerere? Una
lipi la kusema kwa kumlinganisha na viongozi wa zama hizi?
JIBU;
Sioni sababu ya kuwalinganisha viongozi wa awamu tofauti, zama tofauti
zinahitaji viongozi, kumlinganisha Nyerere na Kikwete hiyo itakuwa sawa
kumlinganisha Bismark na Angela Markel.
SWALI;
Unazungumziaje harakati za vyama vya upinzani nchini kupambana na
ufisadi kama wa hivi karibuni wa Tegeta/Escrow? Unadhani vyama hivi vya
upinzani vina dhamira ya dhati kupambana na madudu?Je vitafanikiwa?
JIBU;
Vyama vya upinzani vina nia njema , hii kashfa inayojadiliwa sasa hivi
Bungeni imeletwa na upinzani. Hii vita ya sasa hivi ya Bungeni wanaweza
kushinda, lakini kushinda uchaguzi wa serikali za mitaa ni jambo
lingine.
SWALI;
Kadri ulivyomwelewa hayati Nyerere, unazungumziaje kutokuwepo kwake? Je
unadhani angekuwepo angesaidia vipi kunusuru taifa kwenye kupambana na
ufisadi na kunusuru mchakato wa katiba mpya?
JIBU;
Mwalimu angekuwepo angepinga ufisadi, kuhusu katiba hakuna tatizo kubwa
au naweza kusema hakuna tatizo lolote zaidi ya fujo inayoletwa na
UKAWA.
SWALI; Ukipewa nafasi ya kuwashauri vijana wa sasa wa Tanzania, ungependa wafanye nini kulisaidia taifa lao?
JIBU; Vijana wa Tanzania wafikiri sana kabla ya kuwachagua viongozi.
SWALI;
Unapata tafsiri gani unapoona taasisi za kidini kama kanisa katoliki
likianzisha, kusimamia na kuratibu mchakato wa kumtangaza hayati Mwalimu
Nyerere kuwa Mtakatifu?
JIBU;
Kanisa katoliki ndiyo linataka Mwalimu aitwe lay saint, Mwalimu aliishi
maisha ya uadilifu lakini kama alikuwa mtakatifu hiyo ni kwa Vatican
kuamua.
SWALI;
Unaweza kueleza nini kuhusu siku za mwisho za uhai wa Mwalimu na namna
alivyokuwa akilalamikia ubinafsishaji/uuzwaji wa mashirika ya umma kama
benki ya taifa ya biashara NBC, ukizingatia hali ya ugonjwa wake na uzalendo wake kwa nchi, alikuwa mtu wa namna gani? Alionekanaje nyakati zile?
JIBU; Uuzaji wa mashirika ya umma au ubinafsishaji siyo jambo baya wakati wote.
Swali; una lolote la kumalizia?
Jibu;
Kwa kumalizia, nataka kusema viongozi wachaguliwe kwa uadilifu,
kwasababu ukiwachagua mafisadi, Mungu ataheshimu uteuzi wako, hatabadili
kitu chochote!
Andrew
Nyerere anaweza kupatikana kwa namba 0718- 536281, ikiwa unataka
kuwasiliana na Nova Kambota mwandishi aliyefanya mahojiano haya piga
simu namba 0712-544237, barua pepe; novakambota@gmail.com au tembelea http://novakambota.wordpress.com
إرسال تعليق